Sabaya, wenzake sita kuanza kujitetea leo

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akishuka kwenye gari la Magereza leo Januari 14, 2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ambapo yeye na wenzake sita wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi. Picha na Janeth Mushi.

Muktasari:

Ni kesi ya polisi baada ya washtakliwa hao kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 kwa makosa yanayofanana na ya sasa

Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, wanatarajia kuanza kujitetea leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Hii itakuwa mara ya pili washtakiwa kujitetea katika kesi tofauti lakini zinazohusu makosa yanayoshabihiana.

Katika kesi ya kwanza washtakiwa hao walikumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Akitoa hukumu hiyo Oktoba 15, 2021 Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Arusha, Odira Amworo alisema upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi ya Sabaya na wenzake.

Washtakiwa haoambao safari hii wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, wanaanza kujitetea baada ya kukutwa na mahakama hiyo na kesi ya kujibu katika mashtaka yanayowakabili.

Januari 14, mwaka huu Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Patricia Kisinda alitoa uamuzi mdogo baada ya upande wa Jamhuri kufunga kesi dhidi ya washtakiwa hao.

Akisoma uamuzi huo mdogo, hakimu huyo alisema mahakama imepitia ushahidi wa mashahidi wote 13 na vielelezo 12 vilivyotolewa na Jamhuri kuthibitisha makosa yanayowakabili washtakiwa hao na kujiridhisha kuwa washitakiwa wote saba wana kesi ya kujibu.

“Mahakama imeangalia kila shahidi na vielelzo vyote na imeona washtakiwa wote saba wana kesi ya kujibu.

Alisema kifungu cha Sheria namba 41 (1) cha Sheria ya Uhujumu uchumi na kifungu cha 230 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai, vinawataka washtakiwa wote kujitetea kama ambavyo sheria inaelekeza,” alisema.

Baada ya uamuzi huo mdogo kutolewa, Wakili wa utetezi Mosses Mahuna, akizungumza kwa niaba ya washtakiwa wote, aliieleza mahakama kuwa watakuwa na mashahidi wasiopungua 10 na wote watajitetea chini ya kiapo. Mbali na Sabaya watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matano yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu utakatishaji fedha na kujipatia Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso, huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.

Mengine ni kujihusisha na rushwa na matumizi mabaya ya ofisi.

Katika kesi hiyo Jamhuri ilikuwa na mashahidi 13 na vielelezo 12 na mara ya kwanza watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani Juni 4 mwaka jana na kuanzia Septemba 23 mwaka jana kesi hiyo lilianza kusikilizwa.