Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sakata watu kutoweka, Makonda atoa maagizo polisi

Katibu wa Uenezi, Itikadi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda, akizungumza na mtoto aliyeahidi kumsaidia.

Muktasari:

  • Makonda amesema kauli kuwa  uchunguzi bado unaendelea zinazotolewa na Jeshi la Polisi kuhusu watu waliopotoea au kutekwa, wakati mwingine zinawanyima imani ndugu waliopotelewa na wapendwa wao.

Kigoma. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, amelitaka Jeshi la Polisi nchini Tanzania kutoa taarifa kwa ndugu waliopotelewa na wapendwa wao, badala ya kuwapa majibu ya uchunguzi bado unaendelea pindi wanapohoji suala hilo kwa nyakati tofauti.

 Makonda aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar ea Salaam, amesema majibu kuwa  uchunguzi bado unaendelea yanayotolewa na Jeshi la Polisi hayana afya, kwa sababu yanatengeneza au kuzua sintofahamu kwa wenye ndugu na wananchi.

Ameeleza hayo leo Jumamosi Februari 3, 2024 katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mwanga Center mkoani hapa katika mwendelezo wa ziara yake ya 'back 2 back' ya mikoa 20 awamu ya  pili sehemu ya kwanza, akianzia mkoa wa Kigoma.

"Ombi langu kwa Jeshi la Polisi tunafahamu kazi nzuri mnayoifanya ni pamoja kulinda raia na mali zao, hawa wananchi wanaotaka majibu kuhusu watu waliopotea na nyinyi mnaendelea kufanya uchunguzi, wakati mwingine mnawanyima imani.

"Nimeamua kusema polisi mtoe majibu kwa wakati ili kujenga imani yao kwa wananchi mfano mmoja niliupata Kahama (Shinyanga),mwananchi ameenda kwenye baraza la ardhi la kata kuchukua hukumu aliyoshinda, baada ya kuipata anatekwa, cha ajabu aliowashtaki wameendeleza eneo kwa kujenga kiwanda," amesema Makonda.

Amefafanua kuwa katika maisha kuna watoto ambao familia inaweza kujua ni mtoto mwema lakini tayari ameshajiunga na vikundi vya kihalifu jambo ambalo sio sahihi hivyo polisi wawaambie ndugu husika.

"Tusibaki na neno tupo kwenye uchunguzi, kama kuna taarifa mmeikamilisha muiteni mzazi na kumjulisha kwamba mwanao tumepata taarifa moja, mbili, tatu...ili kama alikuwa mhalifu basi mzazi afahamu, haina afya kila wanapohoji wanaambiwa uchunguzi unaendelea...

"Wapeni majibu yanayowastahili, inawezekana wengine polisi wako wapi, kwa kweli uchunguzi wa kumpata mtu aliyepotea unachukua muda, lakini wazazi toeni ushirikiano na vyombo vyetu vya ulinzi," amesema Makonda.

Amesema inawezekana baadhi ya wazazi wana jambo wanalolijua kuhusu watoto wao lakini kila wanapopata fursa ya kueleza wanatoa wanasema hawajui kabisa, zaidi ya kusema ndugu yao hawakuwa na ugomvi na mtu yeyote.

"Tunatamani kuona Taifa ambalo kila mwananchi ana amani, kama mzazi una taarifa kuhusu mgogoro kati ya mtoto wako na mtu mwingine au ugomvi toeni taarifa polisi kwa kuanzia," amesema.

Makonda amsaidia mtoto aliyeshindwa kwenda shule

Msingi wa Makonda kueleza hayo ulitokana na majibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kigoma (RPC), Phillemon Makungu kueleza bado polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu wakazi wa tatu wa Simbo wilayani Kigoma waliopotea katika mazingira ya kutatanisha.

Awali, akiwa njiani kuekekea Kigoma Mjini amesimama Kata ya Mwandiga eneo la Simbo, ambapo mmoja wa wananchi aliyekuwa na bango lenye picha za watu watatu, alimweleza Makonda kuwa wamepotelewa na ndugu zao hao ambao hadi sasa hawajui wako wapi zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

"Tumeishi katika lindi na mawazo, fikra na vilio visivyoisha ni heri wale ambao ndugu zao wamejua wamefariki lakini sisi hatujui wako wapi, wamepotea tangu Januari 27 mwaka 2023.

"Walikuwa wanauza mikate Jumve lakini tangu walipoenda kazini Januari 27 hawakurejea tena, tumeangaika katika ngazi mbalimbali tunaishukuru CCM na mbunge wamekuwa wakitupa ushirikiano, tunakuomba Makonda utusaidie kuwapata vijana wetu Issa Isango, Abdulkarim Edimo na Jafar Luvanga," amesema mwananchi huyo.

Akijibu suala hilo, mbele ya mkutano wa hadhara, Kamanda Makungu amesema,"ni kweli taarifa zilifika polisi na kufunguliwa kwa jalada la uchunguzi, inasemekana kuna vijana walikamatwa eneo la Jumve bado tunafanya uchunguzi hatujafanikiwa kuwapata," amesema Kamanda Makungu.

Mkoa wa Kigoma unaungana na mikoa ya Shinyanga, Singida na Simiyu ambapo baadhi ya wananchi walijitokeza katika mikutano ya Makonda wakimuomba kuwasaidia kuwapata ndugu zao waliotekwa, huku wengine wakipotea katika mazingira ya kutatanisha, lakini majibu ya polisi katika maeneo hayo walisema uchunguzi bado unaendelea.

Aionya manispaa ya Kigoma Ujiji

Katika hatua nyinginge, Makonda amelionya baraza la madiwani manispaa ya Ujiji akisema wasipobadilika katika utendaji kazi wake, chama hicho kitapeleka mapendekezo katika Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili ivunjwe na kuweka viongozi wa mpito.

Amesema kumekuwa na tabia kwa madiwani na watendaji ya kila mtu kumpa zabuni anayemfahamu sambamba na kuwepo kwa mivutano isiyokuwa na tija inayosababisha mkwamo wa maendeleo katika halmashauri hiyo.

"Wana mivutano isiyokuwa na tija, inayoongozwa na ubinafsi na zaidi ya yote ni upigaji kwa kila mtu kutaka kufanya kazi ya kugawa zabuni, mfarakano huu una wanyima WanaKigoma maendeleo.

Amsaidia mtoto

Katika mkutano huo, Makonda alimsaidia Elhaji Abdallah (10), aliyekuwa akifanya biashara ya ndizi ili kupata kipato cha kukidhi mahitaji ya familia yao baada ya mtoto huyo kumuomba mwenezi kumsaidia kutokana na mazingira magumu anayoishi na mama yake.

Abdallah anayeishi kata ya Gungu Manispaa ya Kigoma Ujiji, alimuomba Makonda msaada ikiwemo kumfadhili ili kuendelea na masomo na kuachana biashara ya ndizi alizokuwa akitembeza ili kupata chochote kitu.

"Nafanya biashara ili kulipa kodi ya nyumba ya Sh 20,000 mama alikuwa ni mgonjwa wa tumbo lake kuvimba, lakini sasa hivi amepata ahueni, huu mtaji nimekopa kwa watu, natakiwa kurejesha baada ya kuuza.

"Nauza ndizi kumlisha mama yangu na wadogo zangu," amesema Abdallah.

Baada ya maelezo Makonda alimuuliza anataka amsaidie nini? Ndipo Abdallah akajibu amsaidie kumsomesha na mama yake apewe msaada, ndilo jambo lake la msingi.

Kutokana na hilo, Makonda alimuita Abdallah katika jukwaa kutamka kuwa watamsomesha kijana huyo, sambamba na viongozi wa wilaya kwenda nyumbani kwa mama yake kwa ajili ya msaada zaidi.

"Chama (CCM), kitamgharamia mama na wewe utasomeshwa na mimi ndio kaka yako, biashara ya ndizi inaishia hapa wewe sio masikini,mama tutampa kodi," amesema Makonda.

Kisha Makonda akafanya harambee ya kumchangia Abdallah ambapo jumla ya Sh 2.2 milioni zilipatikana papo hapo kutoka kwa viongozi wa mkoa wa Kigoma, wananchi huku mwenezi huyo akichangia Sh 1milioni.