Salim Kikeke ang’atuka BBC

Aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Salim Kikeke. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Hadi anaondoka BBC, amefanya kazi kwa miaka 20 akiwa Mtangazaji kinara wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC

Dar es Salaam. Baada ya kufanya kazi kwa muda wa miaka 20 katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) mtangazaji nguli wa habari Salim Kikeke, ametangaza kung’atuka katika shirika hilo.

Kikeke ambaye ni mtangazaji kinara wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, jana Ijumaa Aprili 28, 2023 usiku aliwaaga wafanyakazi wenzake, watazamaji mara baada ya kumaliza kutangaza kipindi cha Dira ya Dunia.

Bila kuweka wazi sehemu anayokwenda, Kikeke amesema anakwenda kufanya majukumu mengine na kwamba katika kipindi chote alichokuwa hapo jijini London baada ya kujiunga na BBC Swahili amekuwa na wakati mzuri tangu akiwa katika redio na kisha kwenye televisheni.

Akiongea kwa bashasha na kujiamini, Kikeke alisema “Mimi ni Salim Kikeke na leo (Jana) ni siku yangu ya mwisho kama mtangazaji Kinara wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, nimekuwa BBC kwa miaka 20, miaka 10 nikiwa kama mtangazaji wa redio na Mhariri  wa tovuti yetu ya BBC Swahili na miaka 10 kama kinara wa Dira ya Dunia TV, mara moja moja nilikuwa nasoma matangazo ya Kiingereza katika matangazo yetu ya BBC Focus on Afrika,” amesema Kikeke na kuongeza.

“Naondoka hapa kwa ridhaa yangu, wakati mwingine hata uwe na uwezo kiasi gani kukaa mahala pamoja kwa muda mrefu unaweza kuharibu kwa sababu ya wewe mwenyewe kuchoka au wengine kukuchoka na ni muhimu kufahamu wakati sahihi wa kuteua kuondoka. Binadamu tumeumbwa na miguu ili tutembee, nimesimama hapa kwa takribani muongo mmoja nadhani ni wakati muafa wa mimi kupiga hatua za matembezi na isingekuwa vyema kuondoka kimyakimya… niko hapa leo(jana) kutoa shukrani zangu za dhati kwa mwenyezi Mungu ambaye aliniwezesha kufika hapa nilipofika  lakini wako wale ambao wamekuwa wakitufuatilia muda wote katika televisheni na kwenye mitandao yetu ya kijamii,” amesema Kikeke.

Pia alichukua nafasi hiyo kuwashukuru wafanyakazi wenzake wa sasa na wa zamani kwa kufanikisha kile walichojaaliwa kwa kadri ya uwezo wao kuweza kufanikiwa.

“Niseme tu sina shaka tutaendelea kuonana na kuwa pamoja kwa njia moja ama nyingine katika majukwaa mbalimbali niwatakie usiku mwema muendelee kuitazama BBC,” amesema Kikeke huku mhariri wake Wazir Khamsini… akimkabidhi keki ya kwaheri na kushukuru kwa kazi aliyoifanya akiwa BBC.

Akimzungumza na kwa niaba ya wafanyakazi wa BBC, mara baada ya kukabidhi keki,  Hamsini amesema waliishi na Kikeke kama familia moja kwamba wataendelea kufanya kazi katika misingi imara aliyoiacha.

Kikeke alipoulizwa na Hamisi, watu watarajie kumuona wapi?  Alisema watu watafahamu baadaye ana kwenda wapi, lakini saizi anarudi nyumbani Tanzania.

Mtangazaji huyo ni miongoni mwa watangazaji vinara kutoka Tanzania kusoma habari katika Televisheni ya Kimataifa na kwa lugha mbili ambazo ni Kiingereza na Kiswahili.

Kikeke alizaliwa Novemba 6, 1978 nchini Tanzania, mbali na BBC amefanya kazi ITV na Chanel Ten.