Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia ataka kufungamanishwa miradi na uzalishaji

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wageni mbalimbali kabla ya kuzindua mchakato wa ukusanyaji maoni kutoka kwa wananchi kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 leo Desemba 9, 2023 katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameainisha mahitaji katika uandaaji wa dira mpya ya 2050, ambayo yanagusa utawala bora, elimu, kilimo, teknolojia, pamoja na kuhakikisha ukuaji uchumi unafungamanishwa na sekta za uzalishaji.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameainisha mahitaji katika uandaaji wa dira mpya ya 2050, akitaja pia changamoto ya kutofungamanisha miradi ya kipaumbele kwa sekta za uzalishaji.

Rais ametoa kauli hiyo leo Desemba 9, 2023 jijini Dodoma, wakati wa mkutano wa kwanza wa kitaifa wa dira ya Taifa ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanzania bara. 

Akizungumza katika hotuba yake ya dakika 40, Rais Samia amesema ni muhimu Taifa kufanya maamuzi sahihi kwa kushirikiana kwenye utekelezaji wa ndoto za miaka 25 ijayo.

“Mfano mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria hadi Dodoma, umejielekeza kwa matumizi pekee, lakini tungeutumia pia kwa miradi ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo  mradi unakopita,” amesema.

Eneo lingine alilolitaja ni upatikanaji wa takwimu kutoka sekta isiyo rasmi ili kutazama mchango wake kwa Serikali, ambapo ameagiza kutazama namna ya kuchochea ukuaji uchumi unaogusa wananchi wengi kupitia ajira. 

Tatu ni tathmini na ufuatiliaji ambayo haikupatiwa umuhimu awali.

“Dira ya mwaka 2025 imeelekeza kila mwaka kufanya tathmini ila tumefanya mara moja tu katikati ya utekelezaji. Inawezekana tungefanya tathmini kila baada ya muda, tungetambua viashiria na kurekebisha mapema na kwenda vizuri zaidi,” amesema.  

Hitaji lingine ni kuongeza mchango wa mashirika ya umma katika kukuza uchumi wa Taifa, ambapo amesema pamoja na hatua zilizoanza kuchukuliwa chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, dira mpya iweke mwelekeo wa uwekezaji na usimamizi.

Sita ni ushiriki wa sekta binafsi ya ndani na nje ya nchi, akitaka sekta binafsi iendelee kuimarishwa na iwe tayari kuimarika ili iwe na uwezo wa kupokea na kushirikiana na wageni kuwekezaji nchini, ili kukuza ajira na uchumi wa Taifa.

Amesema lazima Taifa liweke misingi ili kuwa na jamii yenye kuchukia rushwa, kupinga uchakachuaji mazao, inayolaani ukwepaji kodi, jamii isiyowaibia waathirika wa ajali na jamii ya watu makini, mahili na waadilifu.

Rais Samia amesema kuwa jambo lingine ni kuwa na uwezo wa kubaini viashiria hatarishi na kuweka udhibiti katika matukio yanayotokea na kuathiri mwenendo wa uchumi wa Taifa, akitoa mifano ya ukame, Eli-nino, Uviko 19, vita vya kikanda, mafuta na uhaba wa dola.

Lingine ni kutazama fursa na kudhibiti changamoto zinazotokana na mageuzi ya kiteknolojia duniani ikiwamo sarafu ya kidigitali, akili bandia na teknolojia ya nishati mbadala.

“Tusipokuwa na mipango thabiti masuala hayo yatakuwa changamoto kwa Taifa,” amesema.


Milima, mabonde

Akielezea chimbuko la mipango ya maendeleo, Rais Samia amesema miaka ya 1980/90, Taifa lilipitiwa na changamoto za kiuchumi, kiwango kisichoridhisha cha ukuaji uchumi na Serikali ilichukua hatua, ikiwa pamoja na kupanga mipango ya kukuza uchumi baada ya mwaka 1999 kuzindua Dira ya 2000-2025.

Kupitia dira hiyo, amesema Serikali iliandaa mpango wa muda wa kati katika mfumo wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini (Mkukuta).

Kama hiyo haitoshi, amesema mwaka 2009/10 Serikali ilifanya tathmini ya utekelezaji wa malengo ya dira hiyo, huku ikiandaa mpango elekezi wa muda mrefu wa mwaka 2011/12 hadi 2025/26 uliogawanywa katika vipindi vitatu vya miaka mitano kwenye utekelezaji wake.

Kwa sasa Taifa liko katika kipindi cha miaka mitano ya mwisho ya utekelezaji wa mpango huo elekezi utakaofikia ukomo mwaka 2025.

Utekelezaji Dira ya 2025

Kuhusu utekelezaji wa dira ya 2025, Rais Samia ametaja maeneo yaliyofanyiwa kazi, kikiwemo kilimo ambapo Serikali imefanikiwa kwa asilimia 100 ya utoshelevu wa chakula na inakusudia kufikia asilimia 140 ifikapo 2025.

“Kilichopo mbele yetu ni lishe na usalama wa chakula. Kwa hiyo dira mpya itakayoandikwa itilie maanani kwamba dunia inakabiliwa na changamoto ya usalama wa chakula. Matarajio ni Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula Afrika na duniani kwa ujumla,” amesema.

Kuhusu elimu, amesema dira hiyo imefanikiwa lengo la kuhakikisha watoto wote wa Tanzania wanapata elimu ya msingi na wafike darasa la saba,  kuwawezesha kusoma hadi kidato cha nne bila kulipa ada.

Amesema hatua inayofuata ni kujibu maswali kuhusu elimu yetu na mchango wake katika maendeleo ya mtu mmojammoja na Taifa kwa ujumla.

Kuhusu amani, utulivu na umoja, Rais Samia amesema Taifa limeendelea kuwa na amani na utulivu kwa kipindi chote, akiwasihi wananchi kuendelea kudumisha tunu hiyo huku akisisitiza kuendeleza falsafa yake ya 4R ambazi ni maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi mpya.

“Dira ijayo ikatazame pia hili.  Dira ya 2025 imetuagiza utawala bora ila ijayo tunakwenda mbele zaidi katika kutelekeza eneo hilo,” amesema.

Kuhusu utawala bora, Rais Samia amekiri kuwepo kwa changamoto za kisheria, “Ndiyo sababu niliunda Tume ya haki jinai ili kudumisha utawala bora na utawala wa sheria nchini,” amesema.