Samia ataka riba za mikopo benki kupunguzwa

Samia ataka riba za mikopo benki kupunguzwa

Muktasari:

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemuagiza Gavana wa Benki Kuu (BOT), Profesa Florens Luoga kukaa na Wizara ya Fedha na Mipango kujadiliana namna ya kupunguza kiwango cha riba katika mikopo inayotolewa benki mbalimbali nchini.

Mwanza. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemuagiza Gavana wa Benki Kuu (BOT), Profesa Florens Luoga kukaa na Wizara ya Fedha na Mipango kujadiliana namna ya kupunguza kiwango cha riba katika mikopo inayotolewa benki mbalimbali nchini.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema  riba kuwa juu ni  kikwazo kwa baadhi ya wawekezaji, wafanyabiashara na wananchi wa kipato cha chini kiasi cha kushindwa kukopa katika taasisi hizo za kifedha.

"Viwango vya riba vipo juu mno vishushwe angalau viwe kama asilimia 10 kushuka chini."

"Naagiza Benki Kuu kuanza kutengeneza mazingira ya kuhakikisha wanasimamia benki ndogo ili zitoe mkopo kwa vikundi na wananchi wenye kipato cha chini," amesema.

Pia, amezitaka benki hizo kuanza kutoa mkopo wa muda mrefu ili kuwawezesha wakopaji waanzishe miradi ikiwemo kufungua viwanda, mashamba ya kilimo.

Ameipongeza BoT kwa kuanzisha mfumo jumuishi wa kifedha uliowezesha wananchi kuhusika katika shughuli za kifedha.

"Kutokana na mfumo huu jumuishi leo vijana wengi wamejiajiri katika shughuli za kufanya miamala jambo linalopunguza changamoto ya ajira kwa vijana hao," amesema Rais Samia.

Pia amemtaka Gavana huyo  kuhamasisha wananchi wafanye miamala ya kielektroniki ili kuepuka upotevu wa mapato na uchakavu wa fedha.