Samia ataka wanawake kushikana mikono

Muktasari:

  • Makamu wa Rais nchini Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake walioshika nafasi za juu za uongozi katika nyanja mbalimbali kutambua na kuibua talanta za uongozi walizonazo wenzao.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais nchini Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake walioshika nafasi za juu za uongozi katika nyanja mbalimbali kutambua na kuibua talanta za uongozi walizonazo wenzao.

Amebainisha kuwa hiyo itasaidia kuwajengea ujasiri wanawake wengi watakaoshiriki kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Samia ameyasema hayo leo Alhamisi Machi 4, 2021 katika mkutano mkuu wa tatu wa wanawake katika uongozi uliokwenda sambamba na mahafali ya programu ya   mafunzo ya uongozi kwa wanawake.

Amesema licha ya idadi ya wanawake waliopo katika  uongozi inaongezeka bado inahitajika kufanyika kazi kuhakikisha malengo ya uwiano wa jinsia yanafikiwa.

“Tuacheni hulka mbaya ya adui wa mwanamke ni mwanamke mweziye. Wakati umefika tuungane pamoja na kusema tunaweza, tutashikana na kusaidiana,” amesema Samia.

Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE),  Dk Agrey Mlihuka amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wanawake kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

Amesema wanawake 60 wamehitimu muhula wa tano na sita,“mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo kuwa viongozi kwa kuwapa stadi zote za uongozi ikiwemo kujiamini, kuzungumza, kufanya maamuzi na mambo mengine mengi.”