Samia awagomea wananchi eneo la mwekezaji Kilwa

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi katika mwendelezo wa ziara yake katika mkoani Lindi.

What you need to know:

  • Rais Samia Suluhu hassan amekataa ombi la Mbunge wa Kilwa Kusini, Ally Kasinge la kufuta hati ya kiwanja kinachomilikiwa na Kilwa Yatch Club akisema itasababisha mgogoro na Serikali kuilipa fedha nyingi kampuni hiyo.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amekataa ombi la Mbunge wa Kilwa Kusini (Lindi), Ally Kasinge aliyemuomba afute hati ya umiliki wa ardhi wa kampuni ya Kilwa Yatch Club, akihofia Serikali kupelekwa mahakamani na kuilipa fedha kampuni hiyo.

Rais Samia ametoa majibu leo Septemba 19 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara ukiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ambapo amewataka wananchi wa Kilwa kutorudi nyuma.

“Ndugu zangu, huu ni mgogoro na mwekezaji. Kama mwekezaji alishapewa ardhi na hajasema kushindwa kuwekeza katika eneo lile, kama mnasema tukafute hati, huu ni mgogoro wa uwekezaji, tunapelekwa mahakamani na Serikali inakwenda kulipa fedha nyingi sana,” amesema.

Pia amesema kama eneo hili ni chini ya kilometa moja kutoka bandari hii, amehoji wavuvi hao watakapopelekwa.

“Kwa sababu kwenye bandari hii kuna eneo la wavuvi wadogo na ndio watakaoleta mazao yao, sasa sijui unataka tufute hili eneo ili mpate kitu gani? Watu wa Kilwa badala ya kurudi nyuma, naomba tuwe na mawazo ya kwenda mbele,”

Amemtaka mbunge huyo kutowafurahisha tu wananchi, bali aje na ushauri kama mwekezaji huyo ameshindwa kulitumia eneo hilo, Serikali ichukue hatua.

“Ningefurahi kama ungesema mwekezaji amechukua eneo na hajaliendeleza kwa muda mrefu, mmuhimize aliendeleze na kama kashindwa alirudishe tutafute mwekezaji mwingine, lakini sio tufute haki halafu wavuvi wale warudi kule, halafu iwe nini?” amehoji.  

Wakulima na wafugaji na wanyama waharibifu lipo katika mkoa mzima wa Lindi na wanalichukulia kutafuta suluhisho kitaifa.

Awali akieleza kero hiyo, Mbunge Kasinge amesema kabla ya mwekezaji amesema wananchi walikuwa wakilitumia eneo hilo, lakini mwaka 2003 kwa utaratibu aliouita wa kinyemela alisema eneo hilo lilitolewa kwa Kilwa Yatch Club.

“Wananchi zaidi ya 3000 wamenituma kwako mama, ikikupendeza, uunde tume kuchunguza mgogoro na hatimaye ikikupendeza uweze kufuta hati ya kiwanja 106 ya aneo ambalo Kilwa Yatch Club inamiliki ili wananchi wanaokushahangilia waweze kulitumia eneo hilo bila bugudha yoyote,’ amesema mbunge huyo huku akishangiliwa na wananchi.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameeleza kushangazwa na kero zilizotolewa kwake zikiwa zimepitisha miaka 20 bila kutatuliwa.

“Nilikuwa najiuliza, madai ya fidia ya toka 2003 leo 2023 leo miaka mingapi? Miaka 20 yote Kilwa si mlikuwa na viongozi, si mlikuwa na wabunge wanaowawakilisha? Miaka 20 mnataka leo Rais aje ashughulikie madai ya miaka 20 nyuma? Inashangaza kidogo” amesema.

Huku akimnyanyua aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Suleiman Bungara maarufu kwa jina la Bwege, Samia amehoji kwa nini kero hizo hazikushughulikiwa.

“Wakati mimi naingia bungeni mwaka 2010 miaka 13 iliyopita, Mbunge alikuwa shemeji yangu Bwege, Shemeji yangu huyu na alikuwa na kelele nyingi sana bungeni, sasa nashangaa kwa nini hayakushughulikiwa. Madai ya 2003, mpaka leo 2023?”