Samia: Hadi Desemba mifumo yote ya Serikali isomane

Rais Samia Suluhu Hassan, akizungumza wakati wa uzinduzi wa  Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) leo jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

 Rais Samia Suluhu Hassan amezindua Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC).

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza ifikapo Desemba, 2024 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ahakikishe mifumo yote ndani ya Serikali inasomana.

Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kutoa maelekezo hayo, aliwahi kufanya hivyo Juni 9, 2023 katika Baraza la Biashara Dar es Salaam, akitaka kuharakishwa kwa maboresho yatakayofanya mifumo ya taasisi za umma isomane.

Agizo kama hilo alilitoa tena Agosti 11, 2023 kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kuhakikisha mifumo yote ya Tehama inayotumika ndani ya Serikali inasomana.

“Nilishasema mara mbili hii mara ya tatu natarajia kuona utekelezaji,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Aprili 3, 2024 alipohutubia wakati wa uzinduzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC).

“Mifumo yote ya Tehama isomane, si yule anaenda kushoto, kulia, Mashariki, Magharibi hakuna kusomana, hakuna mawasiliano ndani ya Serikali,” amesema.

Katika maelekezo hayo, ametaka hilo likamilike ifikapo Desemba, 2024 na aliwataka makatibu wakuu wa wizara kuhakikisha wanasimamia utekelezwaji wake.

Mbali na agizo hilo, Rais Samia ameitaka PDPC kuhakikisha inazisajili taasisi zote za umma na binafsi zinazoshughulika na uchakataji na usafirishaji wa taarifa binafsi kabla ya Desemba mwaka huu.

“Pia hakikisheni zinazingatia matakwa ya kisheria katika shughuli hizo, Tume itoe elimu kwa taasisi hizo,” amesema.

Amewataka maofisa wa Tume kufanya kazi ya usajili wa taasisi za umma na binafsi kwa ubora na kuhakikisha wananchi wanaridhika na utunzaji wa taarifa zao.

Hata hivyo, mkuu huyo wa nchi amesema kuna umuhimu wa faragha katika taarifa binafsi, ndiyo maana Serikali imeamua kutunga sheria na kuwa na tume hiyo.

“Ingekuwa taarifa zetu zote ziko wazi na watu wanazijua tusingetazamana usoni, au hii dunia ingekuwa kitu kingine, lakini kwa sababu kila binadamu anahitaji faragha na staha ndiyo maana tumekuja na sheria hii ili kutunza utu wa mwanadamu,” amesema.

Ameeleza baadhi ya taarifa zinaweza kuhujumu jamii na wakati mwingine kusababisha unyanyapaa.

“Unaweza kutoa taarifa ya mtu na ikaleta vurugu kwenye jamii, vita na pengine kuuwa mtu, kwa hiyo kuna kila haja ya kuwa na sheria hii,” amesema.

Kwa upande mwingine, amesema taarifa binafsi ni biashara kubwa kwa kampuni za kimtandao hivyo hapana budi kuzilinda.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema wakati dunia inajenga uchumi wa kidijitali uliozifanya taarifa kuwa bidhaa muhimu, kuzingatia faragha, heshima na utu wa watu ni jambo la msingi.

Ameeleza umuhimu wa Tume hiyo ni hata katika kulinda masilahi ya wawekezaji ndani na nje ya nchi, wawekeze kwa tija.

“Tume inatarajiwa kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria, mazingira haya yatavutia uwekezaji wa ndani na nje kwani wawekezaji watakuwa na uhakika na uwekezaji wao,” amesema.