Samia: Tutajiridhisha kabla ya kukubali chanjo ya corona

Friday May 14 2021
samiapic

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

By Tuzo Mapunda

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema ugonjwa wa Covid-19 umeathiri dunia nzima, ili kukabiliana nao lazima kushirikiana na mataifa mengine lakini Serikali itaendelea kuchukua tahadhari mbalimbali ikiwemo matumizi ya chanjo ya ugonjwa huo.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Mei 14, 2021 katika baraza la Idd lililofanyika leo jioni katika viwanja vya Karimjee mkoani Dar es Salaam.

Alizungumzia suala hilo baada ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) katika risala yao kutaka chanjo ya corona kutolewa kwa hiari huku Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi  akiwataka Waislamu kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam wa afya nchini kuhusu kujikinga na ugonjwa huo.

“Nataka kuhakikishia kwamba tahadhari mlizitoa hapa juu ya chanjo na mengine zitafuatwa kikamilifu na Serikali yenu, hata hivyo hii haina maana kwamba tutapokea kila kitu tunacholetewa au kuambiwa  la hasha lazima na sisi tujiridhishe kwa hiyo.”

“Hata suala la chanjo nalo tutajiridhisha kabla ya kuamua kutumia au kuacha kutumia, hivyo nawasihi Watanzania kutokuwa na hofu yoyote Serikali ipo makini sana katika kushughulikia suala hilo,” amesema Rais Samia.

Advertisement