Saudi Arabia yarejesha tabasamu, zaidi ya Sh3 bilioni zaokolewa

Dar es Salaam. Ujio wa madaktari kutoka Saudi Arabia, warejesha tabasabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo, huku ikidaiwa kuokolewa kwa zaidi ya Sh3 bilioni, ambazo zingetumika kuwapeleka kwenye matibabu nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Septemba 13, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisengi, wakati wa kuwaaga madaktari waliokuja kufanya upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya moyo.
Dk Kisengi mesema kuwa, kwa muda wote tangu Serikali ya Saudi Arabia kuanza utaratibu wa kuwatuma madkatari wake, tayari imetumia Sh3.5 bilioni kwa ajili ya kuhudumia watoto wa Tanzania wenye matatizo ya moyo, ambao wamefanyiwa upasuaji.
“Madaktari kutoka Saudi Arabia umerudisha tabasamu la watoto baada ya kufanyiwa upasuaji ndani ya miaka nne hapa JKCI, hadi sasa watoto 190 wamefaidika na upasuaji wa madaktari kutoka Saudi Arabia tangu mwaka 2019,” amesema.
Amesema kambi ya madaktari hao umesaidia kuokoa fedha ambazo Serikali ya Tanzania ingezitumia kugharamia safari za matibabu nchini India kwa watoto hao.
Dk Kisengi amesema kwa mwaka huu watoto 30 wamefanyiwa upasuaji na madaktari hao kwa kushirikiana na madaktari wa JKCI.
"Tangu 2019, madaktari wenzetu wa Saudi Arabia wamekuwa wakija kila mwaka na kuweka kambi hapa JKCI, ambapo toka wameanza zoezi hilo, tayari wagonjwa 100 wamehudumiwa," amesema Kisengi.
Amesema takwimu zinaonyesha katika watoto 1000 wanaozaliwa, mmoja kati yao, ana tatizo la ugonjwa wa moyo ambapo asipofanyiwa upasuaji kwa haraka, ugonjwa huo unaweza kumsababishia kifo.
Pia Kisengi amesema ujio wa madakta hao umekuwa na tija kwa kuwapa mafunzo na kuwajengea uwezo Madaktari nchini na hivyo matibabu hayo yataendelea kutolewa na maddaktari Wazalendo.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI, Dk Anjella Muhozya, amesema madaktari hao wamekuwa wakifanya upasuaji kwa idadi kubwa ya wagonjwa ambayo ni 30- 35.
"Ufanyaji wa upasuaji kupitia madaktari hawa umepunguza vifo na madhara kuwa madogo na hadi sasa tumeweza kufanya upasuaji hata ambao tulikuwa hatuwezi kuufanya kwa kupitia madaktari hawa," amesema Dk Muhozya.
Dk Muhozya amewaomba madaktari hao kuendelea kuja Tanzania kwa sababu mahitaji ya watoto wenye matatizo ya moyo wanaohitaji huduma ni wengi kwani wagonjwa wanaosubiri kufanyiwa upasuaji, ni zaidi ya watoto 500 kwa sasa.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Saudi Arabia Aloay Abdulsamad amesema madaktari wengi wameshiriki katika kambi hiyo kwa jili ya kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo na kuwafanyia upasuaji kwa wingi.
"Tunahitaji kusaidia watoto na kujitolea ili kuokoa maisha yao na kurudisha tumaini lao tunafahamu kuwa kuna watoto wanauhutaji wa huduma hii ndiyo sababu iliyosababisha tukaja kwa wingi ili kuwapatia matibabu na kupunguza maumivu,"amesema Abdulsamad.
Janeth Njimba mkazi wa Morogoro ambaye amefika JKCI kwa ajili ya upasuaji wa mtoto wake mwenye miaka tisa aliyefanyiwa upasuaji na madaktari kutoka Saudi Arabia.
Amesema baada ya kupewa rufaa ya kufika hapo mtoto wake alifanyiwa na madaktari bingwa na kwa sasa anaendelea vizuri.
"Naomba ushirikiano wa madaktari wa Saudi Arabia uendelee ili kusaidia watoto wengi zaidi wanapokuja kufanya matibabu,"amesema Janeth.