Serikali kuanzisha kamisheni kukabili changamoto za ardhi

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo, Godfrey Pinda akijibu swali katika kikao cha 26 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo Mei 15, 2024. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
- Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza utaratibu wa kuandaa Kamisheni ya Ardhi kukabili changamoto zilizopo.
Dodoma. Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha kamisheni ya ardhi ikilenga kupunguza changamoto za sekta hiyo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Godfrey Pinda amesema hayo leo Mei 15, 2024 akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo.
Mbunge huyo amehoji Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mamlaka maalumu ya kusimamia sekta ya ardhi ili kuondoa changamoto zinazojitokeza.
Naibu Waziri Pinda amesema ni mpango wa wizara kuwa na mamlaka kamili inayosimamia masuala ya ardhi na mchakato wake umeanza.
“Tumeshaanza mchakato, tunaanzisha kamisheni ya ardhi ambayo itaenda kufanya kazi sawa na ilivyo kwa mamlaka nyingine kama idara ya maji, Tarura (Mamlaka ya Barabara Mijini na Vijijini),” amesema.
Amesema kamisheni ya ardhi itakuwa na kamishna na mtiririko wa uongozi utaenda hadi vijijini kwa kuwa na wawakilishi wa kamisheni hiyo.
Katika swali la msingi, mbunge huyo amehoji Serikali ina mkakati gani ya kupanga matumizi bora ya ardhi kutokana na kasi ya ongezeko la watu nchini.
Akijibu swali hilo Pinda amesema hadi sasa, jumla ya vijiji 4,024 kati ya 12,318 vilivyopo nchini vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.
“Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha vijiji vyote nchini vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi,” amesema.
Amesema miongoni mwa mikakati inayoendelea kutekelezwa ni kuzihimiza mamlaka za upangaji kutenga fedha kwa ajili ya uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji.
Ametaja mikakati mingine ni kuendelea kutenga bajeti kwa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, ili iweze kuandaa, kuwezesha na kusimamia upangaji wa matumizi ya ardhi.
Mikakati mingine ni kuhamasisha wadau kuchangia upangaji wa matumizi ya ardhi na kubuni miradi ambayo inawezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi.
“Wizara ilibuni na kutekeleza mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki (LTIP) ambao umelenga kuwezesha uandaaji wa mipango 1,667 ya matumizi ya ardhi katika kipindi cha miaka mitano,” amesema.
Pinda amesema Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imetenga Sh5.04 bilioni kwa ajili ya kuiwezesha tume kuendelea kupanga matumizi ya ardhi.
“Azma ya Serikali ni kupanga miji na vijiji vyote ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya ardhi linalochangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la watu,” amesema.
Ametoa rai kwa wabunge, kuhakikisha halmashauri zinaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kupanga miji na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji.