Serikali kuchunguza dawa za kulevya kuwekwa kwenye shisha
Muktasari:
- Wakati matumizi ya dawa za kulevya yakipungua, Serikali imetangaza kuchunguza madai ya kuwekwa dawa za kulevya kwenye shisha huku kukiwa na matumizi ya dawa za hospitali kulewa na ‘mateja’ zaidi ya 12,000 wajisalimisha.
Dodoma. Wakati matumizi ya dawa za kulevya yakitajwa kupungua nchini, Serikali imekiri kwamba bado kuna changamoto ya baadhi ya watu kutumia dawa za binadamu kama mbadala wa dawa hizo haramu ikiwemo dawa aina ya valium.
Pia, Serikali imeeleza kwamba inafanya uchunguzi ili kubaini kama dawa za kulevya zinawekwa kwenye shisha katika baadhi ya kumbi za starehe.
Mwaka 2016, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika futari iliyoandaliwa kwenye msikiti wa Khoja Shia Ithnaasheri, Mtaa wa Indira Gandhi jijini Dar es Salaam, alipiga marufuku uvutaji wa shisha huku mkuu wa mkoa wa Dar es salaam wakati huo, Paul Makonda akitangaza marufuku uvutaji huo hadharani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 25, 2023 jijini hapa katika maadhimisho ya wiki ya sheria, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerald Kusaya amesema biashara na matumizi ya dawa za kulevya imepungua nchini.
Amesema katika kipindi cha Desemba 2021 hadi Desemba 2022, wameweza kukamata jumla ya dawa za kulevya 11,990 za aina mbalimbali.
Kusaya amesema katika dawa hizo, iliyokuwa ikiongoza kwa kiwango kikubwa ni bangi kilogramu 6,900, mirungi kilogramu 4,300, huku heroine na cocaine zikiwa ni chache.
Pia, amesema wameweza kukamata kemikali bashirifu zaidi ya lita 85,000 zilizokuwa zikitaka kuingizwa nchini.
Hata hivyo, amekiri kuwa bado kuna changamoto ya matumizi ya dawa za binadamu zenye asili ya kulevya kutumika kama mbadala wa dawa za kulevya.
Amesema dawa ya Ephedrine inatumika kutibu kifua, Ketamine inatumika kuondoa maumivu kwenye operesheni na ipo ya aina mbili ya vidonge na maji, Tramadol inatumika kuondoa maumivu na valium kutibu mafua na kupata usingizi.
“Wanatumia kwa sababu wanakosa kile anachokihitaji, hizi dawa zikitokea bahati mbaya matumizi yakawa makubwa mtu anaweza kupoteza maisha,” amesema Kusaya.
Kuhusu matumizi ya shisha, Kusaya amesema wanafanya uchunguzi kuhusu kutumika ndivyo sivyo.
Amesema bado wanaendelea na uchunguzi huo na watatoa majibu hivi karibuni.
“Shisha sio madawa ya kulevya ila ikatokea mtu akaweka dawa za kulevya kwenye shisha hilo ni kosa. Sisi hizo taarifa tunazo tunaendelea kuzifanyia kazi kwa kutumia mamlaka husika,” alisema Kusaya.
Katika hatua nyingine, Kusaya amesema jumla ya watu 12,800 wamejisalimisha na kuamua kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.
“Watu hao wanapatiwa dawa aina ya Methodine katika vituo 15 vilivyopo nchini hasa waliokuwa wakitumia heroine, cha msingi matumizi yamepungua ila mapambano ndio yanaendelea. Sasa tunachofanya Serikali ni kuwa mbele yao ili kuwalinda wasirudi tena kwenye matumizi,” amesema Kusaya.