Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kufanya tathmini madhara ya mvua Hai

Muktasari:

  • Serikali imeanza kufanya tathmini ya maeneo ya yaliyoathiriwa na upepo mkali uliombatana na mvua za mawe iliyoathiri zaidi ya nyumba 15 na ekari 20 za mashamba ya kahawa na migomba katika kata ya Machame Mashariki na Kijiji cha Lyamungo kati Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro.

Hai. Serikali imeanza kufanya tathmini ya maeneo ya yaliyoathiriwa na mvua ya mawe iliyoambatana na upepo mkali na kuathiri zaidi ya nyumba 15 na ekari 20 za mashamba ya kahawa na migomba katika kata ya Machame Mashariki na kijiji cha Lyamungo katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali ilinyesha juzi Januari 19, 2024 na ilidumu kwa zaidi ya saa moja na kuleta taharuki kwa wananchi wa wilaya hiyo baada ya kuangusha miti mikubwa, kimuni, migomba na mahindi mashambani huku majani ya migomba na mahindi yakichanwachanwa na mvua hiyo ya mawe.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amiri Mkalipa amesema mvua hizo zimesababisha madhara makubwa katika wilaya hiyo na kwamba tayari maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo yameanza kufanyiwa tathmini na misaada ya kibinadamu kutolewa kwa waathirika.

“Tulipata mvua iliyoambatana na upepo mkali katika baadhi ya kata za wilaya hii, hasa kata ya Machame Mashariki, kijiji cha Lyamungo Kati, athari zilikuwa kubwa. Miti mingi ilianguka na hata barabara ya Moshi – Arusha ilijifungwa kwa muda, nguzo za umeme nyingi zilianguka kwa sababu ya upepo mkali.

“Kwenye mashamba tulipata athari kubwa kwa sababu ilinyesha mvua ya mawe ambayo iling'oa migomba na parachichi lakini timu yetu ya tathmini inaendelea kufanya kazi, tutaendelea kutoa taarifa, mpaka sasa ekari zaidi ya 20 za migomba, kahawa na parachichi zimeharibiwa na mvua hizi,” amesema.

Mkuu huyo wa wilaya ameongeza: “Serikali tumepanga na tayari vikao vya maafa wilaya vinaendelea, tunamshukuru Mungu hali hiyo haikuleta vifo wala majeruhi, hivyo Serikali ya wilaya tumejipanga na timu ya tathmini inaendelea kwa kufanya kazi ya tathmini ili tupate tathmini ya kina ili wenzetu wa malamka za juu waweze kuzipata.”

Amesema kwa wale ambao waliopata athari kubwa, misaada ya kibinadamu imeshaanza kupelekwa kwenye maeneo husika kwa kupitia kamati zao za maafa za wilaya.

Wakizungumzia athari za mvua hizo, wananchi wa kitongoji cha Marukeni,  kijiji cha Nshara, wilayani humo wamesema mvua hizo zimesababisha vilio kwa kuwa zao la ndizi na kahawa limekuwa ni msaada mkubwa kwao kwa kuwa walikuwa wakiuza na kujipatia kipato cha kuendeshea maisha na kusomeshea watoto.

Ewiri Mwanga, mkazi wa kitongoji cha Marukeni amesema mvua hiyo imeleta maafa kwa wananchi kwa kuwa mazao waliyokuwa wakitegemea ndiyo yalimeathiriwa na huenda wakapata baa la njaa.

“Ilikuwa majira ya saa tisa mchana ambapo upepo mkali  ulivuma ukiwa umeambatana na mvua ya mawe makubwa ya barafu, upepo ulikuwa mkali sana na ulidumu  kwa zaidi ya saa moja, hali ambayo ilisababisha taharuki kubwa kwa wananchi, wengine tulibaki tukisali maana tulikuwa hatujui hatima yetu.

"Miti, migomba mingi ilianguka, madhara ni makubwa na hata huko tunakokwenda hakutakuwa na chakula maana hizi ndizi ndio tulikuwa tunazitegemea kwa chakula na biashara,” amesema Mwanga.

Kwa upande wake, Lilian Nkya, mkazi wa Marukeni amesema mazao yaliyoathiriwa na mvua hizo ni yale ambayo walikuwa wakiyategemea kwenye biashara ambayo yalikuwa yakiwapatia kipato na wakati mwingine kuwasaidia kulipa marejesho ya mikopo, hivyo anaiomba Serikali ione namna ya kuwasaidia.

Mkazi wa Kijiji cha Nshara, Manase Nkya amesema “hii mvua na upepo imeathiri mazao mengi, tunavyoongojea hivi mashamba yangu ekari nne yenye migomba yameharibiwa kabisa, hapa sina kitu kabisa. Kwa hiyo hapa ni njaa, maana hatuna msaada mwingine kabisa labda Serikali itusaidie maana tulikuwa tunategemea hizi ndizi na kahawa itupatie kipato,” alisema..

Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe ametoa pole kwa wananchi wote waliokumbwa na maafa hayo wilayani humo na kuwaomba wawe na subira wakati Serikali ikiangalia namna ya kuwasaidia.

“Naomba tuwe watulivu wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya maeneo yaliyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu,” amesema mbunge huyo.