Serikali kufutia leseni vyuo 124 vya udereva

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani kimevifungia vyuo vya mafunzo ya udereva 124 kutokana na kukosa sifa ya kutoa taaluma hiyo.

Arusha. Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani kimevifungia vyuo vya mafunzo ya udereva 124 kutokana na kukosa sifa ya kutoa taaluma hiyo.

Mbali na hatua hiyo, pia limepanga kuzifutia lesseni ya uendeshaji wa mafunzo hayo ili kuanza mchakato upya wa maombi watakapokidhi vigezo.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Ramadhani Ng'anzi alipokuwa akikagua Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kinachotoa mafunzo ya udereva.

Alisema kuwa chanzo cha ajali nyingi za barabarani, wamebaini kinatokana na uzembe wa madereva wanaotengenezwa na vyuo ambavyo havina sifa, na kwamba wameanza na ukaguzi wao kujiridhisha na ubora wa elimu itolewayo.

"Tuko hapa Chuo cha Ufundi Arusha, kwanza kutembelea eneo lao la mafunzo lakini pia walimu na vifaa vyao, hii ini sehemu ya kaguzi zinazoendelea nchini na bahati nzuri wao wamekidhi vigezo, kikubwa wawafuatilie mawakala wao waliopo mikoani kuepuka rungu hili," amesema bosi huyo wa trafiki.

Alisema kuwa katika kaguzi za mwezi Agosti, wamefanikiwa kukagua vyuo 230 ambapo 124 vimekosa sifa na wamefungia ambapo wanatarajia kuvifutia kabisa lesseni.

"Vyuo 106 pekee ndio zenye sifa na vinaendelea na kazi, wana eneo la kutosha na vitendea kazi, vifaa lakini pia walimu, na baada ya vyuo tutaanza kufanya operesheni maalum ya kukagua lesseni na vyeti vya madereva na visivyo na sifa tutavifuta ili kuweka nidhamu ya tasnia hii nzima," amesema Ng'anzi.

Kwa upande wake Mkuu wa ATC, Mussa Chacha, amesema kuwa wanayofuraha kutembelewa na ugeni huo sambamba na kupata sifa za kuendesha mafunzo ya udereva nchini.

"Chuo chetu kwa upande wa uhandisi wa magari tumeweka pia mafunzo ya udereva ambayo yanatolewa na mawakala wetu katika matawi yaliyoko mikoa mbali mbali nchini, ambapo tunasisitiza uweledi na ufanisi kazini kwa lengo la kutengeneza madereva bora watakaoingia sokoni na kupunguza ajali kwa watu wetu," amesema Chacha.

Mmoja wa wanafunzi wa udereva chuoni hapo, Merry Mwita, amesema kuwa ndoto yake ni kuendesha watalii, tatizo kubwa barabarani ni ujuaji na ubabe wa baadhi ya madereva wanapokuwa barabarani, hali inayopelekea ajali nyingi kutokea.

"Hapa naona msisitizo wa nidhamu barabarani kwani madereva wengi wanazijua sheria, kanuni na taratibu lakini kiburi au kuona sifa katika uvunjaji wa sheria ni kama ufahari kwao, ikiwemo mwendo kasi, kuyapita magari mengine au hata kutokufuata alama za barabarani na taa zake"

Alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuunda kifurushi cha kupumzisha baadhi ya madereva watakaobainika kusababisha ajali kwa uzembe wafutiwe lesseni kwa miezi sita au mwaka kulingana na ukubwa wa kosa.