Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Trafiki wamaliza utata wa uhakiki wa leseni

Muktasari:

Utata uliozuka kutokana na agizo la Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi kuwataka madereva kuhakiki leseni kwa kuwa na vyeti umepatiwa ufafanuzi.

Dar es Salaam. Utata uliozuka kutokana na agizo la Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi kuwataka madereva kuhakiki leseni kwa kuwa na vyeti umepatiwa ufafanuzi.

Baadhi ya madereva kupitia mitandao ya kijamii walihoji sababu za kutakiwa kutembea na vyeti vya udereva kwa ajili ya uhakiki.

Lakini, Kamanda wa kikosi hicho nchini, Fortunatus Musilimu akizungumza na Mwananchi jana alisema lengo la uhakiki ni kuhakikisha utaratibu wa kupata leseni unafuatwa kwa mujibu wa sheria.

“Sijasema watu watembee na vyeti, sheria inasema dereva anatakiwa kutembea na leseni. Utaratibu wa kupata leseni unakutaka kwanza ukasomee udereva, kisha utapata leseni daraja D, utakaa nayo miaka mitatu,” alisema.

Kamanda Musilimu alisema, “Baada ya miaka mitatu utabadilisha, sasa kwa kuwa umeshapata uzoefu, unatakiwa ukasome tena ili upate daraja E ambalo utaruhusiwa kuendesha malori. Baada ya miaka mitatu utasoma tena na hapo tutakupa daraja C ambalo nalo lina madaraja 1, 2 na 3. Hiyo ni kwa ajili ya kuendesha magari ya abiria.”

Kuhusu Watanzania na wageni wanaotoka nje ya nchi, alisema itategemea wametoka nchi zipi.

“Kama mtu ametoka nchi zilizotawaliwa na Uingereza atakuwa anafuata (Mkataba wa Vienna) Vienna Convention ambayo inataka magari yapite kushoto, huyo tutampa leseni. Wale wanaotoka nchi za magari yanayopita kulia wanafuata Geneva Convention, hao hatuwapi hadi wawe na leseni ya kimataifa,” alisema.

Alisema hata madereva wanaotoka Zanzibar watakaguliwa leseni zao na kupewa kulingana na daraja alilopo.

Kamanda Musilimu alisema kwa wanaotoka nchi za magari yanayopita kushoto watatakiwa kuwa na leseni za kimataifa au wasome upya.

Alisema sababu ya uhakiki huo ni mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani iliyotungwa mwaka 1965 na kufanyiwa mabadiliko mwaka 1996. “Awali sheria haikumlazimisha mtu kwenda shule ili apate leseni. Mwaka 1996 ndipo ikasema ni lazima dereva akasome. Sasa miaka 30 imepita kuna madereva wamepata leseni lakini hawakuwahi kusoma,” alisema.

Alisema, “Lengo ni kuwasaidia hawa waliopata leseni bila kusoma ili wafuate utaratibu. Halafu kuna madereva hawana leseni mahsusi kwa magari wanayoendesha. Mtu ana daraja E, lakini anaendesha gari la abiria, huyo naye tutataka afuate utaratibu.”

Alisema uhakiki huo ni rafiki kwa madereva na hakuna atakayekamatwa, bali watasalimisha leseni zao ili wakasome kwanza.

Kutokana na utata uliokuwepo awali, miongoni mwa waliohoji uhakiki huo ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume aliyekosoa utaratibu huo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter akisema uko kinyume cha sheria.

“Lazima tuelewane maana sote ni Watanzania, lakini kwa sasa hivi tutaikosoa Serikali inayoendeshwa kwa amri na si kwa sheria. Hakuna Sheria inayosema lazima utembee na cheti cha kufaulu driving school. Sheria inataka uwe na driving license (leseni ya udereva) kama unaendesha chombo cha moto,” alisema Karume katika Twitter.

Alisema, “Leseni unapewa na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) baada ya kupasishwa na Polisi na baada ya kwenda driving school (shule ya udereva). Polisi wanasema wanaamini cheti cha driving school lakini hawaiamini leseni inayotolewa na Polisi wakishirikiana na TRA.”

Akizungumza na waandishi wa habari wiki hii, Kamanda Musilimu alisema watafanya uhakiki wa kina wa leseni za udereva na kuwataka madereva kujaza fomu itakayowekwa kwenye ofisi za makamanda wa usalama barabarani wa mikoa na vituo vya mabasi.

Alisema leseni 225 zimekamatwa na zimezuiliwa kutokana na madereva kutokuwa na vyeti vya shule au kutokusoma kabla ya kupata leseni.

Kutokana na utata uliokuwepo, katika chuo cha Veta baadhi ya madereva walikwenda kuuliza utaratibu wa kupata mafunzo ya udereva licha ya kuwa na leseni, lengo likiwa kupata vyeti.

Baadhi ya watendaji wa kampuni walikwenda Veta kujua utaratibu wa mafunzo kwa madereva wao ambao hawana vyeti.

Kaimu mkuu wa chuo hicho, Hermenegild Msue alisema kuna mwamko wa watu kuhitaji mafunzo lakini bado wanaendelea kusajili ndipo wajue ni kozi za aina gani wawapatie.

Mratibu wa kozi fupi chuoni hapo, Mashaka Kasala alisema wamejipanga ili watakaohitaji mafunzo wayapate kulingana na programu zilizopangwa na Veta.

Alisema wanatarajia kuwa na darasa Julai 30 walengwa wakiwa madereva wa magari ya abiria zaidi ya 100.