Serikali kulibeba sakata la wakulima, wafugaji Nachingwea

Muktasari:
- Rais Samia ameonyesha kusikitishwa na wananchi kuuawa na wanyama wakali huku akisema suala hilo litachukuliwa hatua zaidi na Serikali Kuu.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema migogoro ya wakulima na wafugaji na athari za wanyama waharibifu wilayani Nachingwea ni miongoni mwa mambo yatakayoshughulikiwa na Serikali Kuu.
Kauli hiyo ya Rais Samia imekuja baada ya hatua mbalimbali za Wilaya na Mkoa wa Lindi kushindwa kufua dafu juu ya changamoto hizo.
Kero ya wanyama wakali na migogoro ya wakulima na wafugaji imeibuliwa na Mbunge wa Nchingwe, Amandus Chinguile aliyesema pamoja na juhudi mbalimbali kunahitajika hatua zaidi.
“Kama sijasema kadhia ya ufugaji wananchi hawatanielewa na kura hizi nazitaka, lazima niseme walichonambia niseme. Tunajua kuwa nchini wapo wafugaji na wakulima, lakini katika maeneo yetu sisi ni wakulima, kuna mifugo mingi kwenye maeneo yetu inayoathiri mashamba yetu,” amesema.
Rais Samia ameeleza hayo wilayani Nachingwea leo, Septembea 17, 2023 alipohutubia wananchi wa wilaya hiyo katika mwendelezo wa ziara zake.
Katika hotuba yake hiyo iliyochukua dakika sita, ameeleza kusikitishwa na hatua ya wananchi 10 kuuawa na tembo kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023.
“Nasikitishwa sana kwamba hapa Nachingwea kwamba kutoka 2021 hadi 2023 kiasi cha watu 10 wameshauawa na wanyama wakali hii si sura inayopendeza,” amesema.
Ameeleza kwa kuwa inaonekana katika ngazi ya Wilaya na Mkoa limeshindikana, kikao cha kitaifa kitafanyima kushughulikia hilo, kadhalika na lile la migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Tunakwenda kulikomesha kadhia hii ya wakulima kuuawa kwa sababu ya wafugaji, kutoa umuhimu zaidi kwa uhai wa ng’ombe kuliko wa binadamu,” amesema.
Awali, akizungumza katika mikutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa amesema kila changamoto wizara husika zitashughulikia kwa maelekezo ya Rais Samia.
“Sisi mawaziri wako vijana tutakwenda kukaa kwa pamoja kuona namna tunakavyoshughulikia matatizo haya kwa maelekezo yako,” amesema.