Serikali kupangua madaktari bingwa hospitali za mikoa

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza bungeni. Picha na mtandao
Muktasari:
- Serikali imesema inatarajia kugawa upya madaktari bingwa katika hospitali za rufaa za mikoa kutokana na upungufu uliopo, wakati ikiendelea kuzalisha kwa wingi wataalamu hao kwa wingi kupitia utaratibu ulioanzisha wa Samia Super Specialist Program.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kutokana na upungufu wa wa madaktari bingwa katika baadhi ya hospitali za rufaa za mikoa, wizara yake imelenga kugawa upya wataalamu hao ili kukabiliana na changamoto ya utoaji huduma.
Waziri Ummy, ameyasema hayo leo Jumanne, Aprili 18, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akifafanua maswali aliyoulizwa na Mbunge wa Tabora mjini, Emmanuel Mwakasaka katika mkutano huo ambapo ameeleza kuwa wamefanya tathmini za haraka na kugundua upungufu wa madaktari bingwa katika hospitali za rufaa za mikoa.
"Tumefanya tathmini za haraka ya madaktari bingwa na tumegundua kuwa baadhi ya hospitali za rufaa za mikoa kuna madaktari wengi kuliko hospitali zingine, hivyo tunafanya ugawaji mpya wa madaktari ili kukidhi mahitaji katika kila hospitali wakati tunasubiri madaktari walioenda kusoma," amesema Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa mwaka huu wizara imepata kibali cha ajira mpya, hivyo imelenga kuajiri madaktari bingwa katika hospitali za rufaa za mikoa hasa zile zenye changamoto ya upungufu wa madaktari hao.
Mbali na hayo waziri Ummy amesema serikali inaendelea na mkakati wa kusomesha wataalamu kwa mfumo wa kujiendeleza katika fani za kibingwa na wanapomaliza watarudi katika vituo vyao na kuendelea na majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
"Serikali ya awamu ya sita imetenga zaidi ya Sh8 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mpango wa 'Samia Super Specialists Program' ambao utasomesha madaktari bingwa zaidi ya 400 ndani na nje ya nchi kwa muundo wa jumuishi yaani madaktari bingwa, muuguzi na mtu wa usingizi," amesema Ummy.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel ameeleza juu ya uhaba wa madaktari bingwa katika hospitali ya Kitete mkoani Tabora, akisema kuwa tayari wizara hiyo imepeleka madaktari sita kusoma.
Amesema kati ya madaktari hao, wawili wanasomea ubingwa wa magonjwa ya ndani, daktari wa magonjwa ya kinywa, sikio na koo mmoja, daktari bingwa wa mionzi mmoja, daktari wa magonjwa ya dharura mmoja na daktari bingwa wa afya ya wamama na uzazi mmoja.
"Hospitali ya rufaa ya mkoa ya Kitete hadi sasa ina jumla ya madaktari bingwa watano ambapo daktari wa afya ya uzazi mmoja, madaktari bingwa wa watoto watatu na daktari bingwa wa upasuaji mmoja," amesema Dk Mollel.