Serikali kurudia uthamini wa mali Bonde la Mto Msimbazi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Anjelina Mabula akijibu swali la mbunge wa Kinondoni Tarimba Abbas leo Ijumaa April 14,2023 bungeni. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
- Serikali imesema kwa sasa inaendelea kufanyia kazi malalamiko ya uthamini wa mali katika Bonde la Msimbazi kutokana na malalamiko yaliyojitokeza.
Dodoma. Serikali imesema kwa sasa inaendelea kufanyia kazi malalamiko ya uthamini wa mali katika bonde la Msimbazi kutokana na malalamiko yaliyojitokeza.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Aprili 14, 2023 bungeni wakati Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Anjelina Mabula alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Kinondoni Tarimba Abbas.
Mbunge huyo ameuliza iwapo Serikali itakuwa tayari kufanya mapitio ya tathmini kwa Wananchi wanaopisha Mradi wa Kuboresha Bonde la Mto Msimbazi baada ya kubainika kuwa na mapungufu.
Waziri Mabula amesema kufuatia malalamiko ya wananchi yaliyojitokeza kuhusu uthamini wa mali katika eneo la Bonde la Mto Msimbazi, Serikali kupitia Wizara yangu na Ofisi ya Rais – Tamisemi inaendelea kufanyia kazi malalamiko hayo kabla ya kuidhinishwa kwa taarifa za uthamini.
Waziri Mabula amesema zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi litafanyika baada ya malalamiko hayo kupatiwa ufumbuzi na Serikali kujiridhisha.