Serikali kutoa Sh300mil kuchangia mfuko wa maji
Muktasari:
- Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfuko huo, alisema mbali ya Serikali kutoa fedha hizo lakini pia itawashawishi wahisani wengine kuchangia mfuko huo.
Dar es Salaam. Serikali itakuwa inatoa Sh300 milioni kila mwaka kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa Ufundi wa Maji (WTF),ambao una lengo la kuwawezesha wanafunzi ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwaendeleza kumaliza masomo yao katika nyanja hiyo.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfuko huo, alisema mbali ya Serikali kutoa fedha hizo lakini pia itawashawishi wahisani wengine kuchangia mfuko huo.
Alisema wanafunzi ambao si wa elimu ya juu wengi wamekuwa wakishindwa kumaliza masomo licha ya kuwa na uwezo mkubwa kitaaluma kutokana na wazazi wao kutokuwa na uwezo kifedha.
Profesa Magembe alisema kuwa mahitaji halisi ya watalaamu katika sekta ya maji ni watu 3,000 lakini taasisi hiyo muhula wa masomo kwa mwaka 2012/13 ilidahili wanafunzi 358 kiwango ambacho ni kidogo ukilinganisha na mahitaji halisi.
Maghembe alisema ni vema wadau wa maji na wananchi wengine wa kawaida wakachangia mfuko huo na alitaka kitolewe kipaumbele kwa wanafunzi wa kike kutokana na uchache wao katika sekta hiyo.