Serikali, wadau kuwapa wanawake ujuzi wa teknolojia

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima katika hafla ya ugawaji wa kompyuta mpakato kwa mabinti wanufaika wa mradi wa 'Binti Digital' leo jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia kuendelea kukua duniani kote, bado wanawake wameonekana kubaki nyuma.

Dar es Salaam. Katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika matumizi ya teknolojia, Serikali imeweka mkakati wa kushirikiana na wadau kutoa elimu ili kufikia usawa wa kijinsia katika uga huo.

Hayo yamesemwa leo Juni 3 jijini Dar es Salaam  na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima katika hafla ya ugawaji wa kompyuta mpakato kwa mabinti wanufaika wa mradi wa 'Binti Digital.'

Amesema Tanzania pia imekuwa na sera mahususi katika kuhakikisha usawa wa kijinsia na masuala mbalimbali ikiwamo yale yanahusu sayansi na teknolojia.

"Juhudi hizi zimesababisha ongezeko kubwa la uandikishwaji wa wasichana shuleni katika miaka ya hivi karibuni, jambo ambalo ni muhimu katika kufikia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana.”

Pia, amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema teknolojia ni muhimu katika kukuza uchumi, ubunifu na kuboresha maendeleo ya jamii na Tanzania kama ilivyo nchi nyingine inashuhudia mapinduzi ya kidijitali yanayotoa fursa kwa wanawake na wanaume katika nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa vijana hasa mabinti waliopata mafunzo hayo ya teknolojia kutumia fursa zinazopatika kutokana na ukuaji wa teknolojia katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Mwakilishi Mkazi wa UN Women, Peterson Magoola amesema ili kufikia usawa wa kijinsia katika masuala ya teknolojia, wameanzisha programu mbalimbali ikiwamo ya 'Binti Dijital' ambayo imelenga kuwawezesha mabinti wenye umri kati ya miaka 17 hadi 25 kwa kuwapatia mafunzo yatakayowawezesha kufanya ubunifu katika masuala ya teknolojia.

Amesema kwa mwaka 2023 programu hiyo iliwafikia mabinti zaidi ya 100 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

"Baadhi yao baada ya kupata mafunzo wamejiajiri, kuajiriwa na hata kuja na bunifu wa aina mbalimbali,"

Ameongeza kuwa mradi huo utafanyika tena kwa awamu nyingine na sasa unatarajiwa kuwanufaisha mabinti waliopo katika maeneo ya vijijini.

Mtaalamu wa kuwawezesha wanawake kiuchumi kutoka UN-Women, Lilian Mwamdanga amesema utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa asilimia 90 ya kazi zote zinahitaji kuwa na maarifa kuhusu masuala ya teknolojia, hivyo uwepo wa mafunzo hayo yatasaidia kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake.

Mkuu wa Idara ya Uhusiano katika balozi wa Ubelgij hapa nchini, Fanny Heyler amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwa na kuimarika hapa nchini.