Prime
Serikali yachunguza watumishi wanaojipatia uhamisho bandia
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene
Muktasari:
- Serikali inachunguza matukio ya baadhi ya watumishi wanaohama kwenye maeneo yao ya kazi kwa kughushi saini za makatibu wakuu wa Tamisemi na Utumishi na atakayebainika atafukuzwa kazi.
Geita. Serikali inachunguza matukio ya baadhi ya watumishi wanaohama kwenye maeneo yao ya kazi kwa kughushi saini za makatibu wakuu wa Tamisemi na Utumishi na atakayebainika atafukuzwa kazi.
Akizungumza juzi na watumishi wa halmashauri mbili za Wilaya ya Geita, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema tayari Serikali imeanza kuwakamata watu wanaojifanya wapo Utumishi wanaoghushi saini za watendaji hao kujipatia kipato.
Alisema watumishi watakaobainika kutoa rushwa ili wahamishwe na kushirikiana na watu wanaoghushi saini za viongozi kuhalalisha uhamisho, wakikamatwa watafukuzwa kazi na kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria.
“Tunaendelea na uchunguzi wa kina, tumegundua kuna watu wanafanya uhamisho feki ambao si wa katibu mkuu Utumishi, tumeanza kuwakamata na tutaendelea kuwakamata. Wapo wanaotoa rushwa kwa watu wanaojifanya wako Utumishi (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) na Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ili wahamishiwe kwenye taasisi kubwa, wote hawa wanamdanganya mwajiri na hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Simbachawane.
Waziri Simbachawene alisema uhamisho huo wa uongo na feki umebainika baada ya watu hao kushindwa kuhamisha mshahara wa mtumishi kutoka alipokuwa akifanya kazi awali kwenda kwenye taasisi au eneo jipya alilolahamishiwa.
“Kuhamisha mshahara si jambo rahisi na hapa ndio tumewakamatia,” alisema.
“Tunachunguza waliotoka walipitia wapi na tukigundua tutawarejesha walikotoka, yule aliyehama kwa uhamisho wa uongo na ameshindwa kuhamisha mshahara, arudi alikotoka mapema kabla hatujachukua hatua ya kumtafuta, vinginevyo atafukuzwa kazi,” alionya.
Kibano Tasaf
Katika hatua nyingine, Simbachawene aliagiza utoaji wa fedha kwa watu wasio na sifa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini (Tasaf) badala yake fedha hizo zipangiwe kazi nyingine.
Agizo hilo alilitoa baada ya kupokea taarifa ya Mkoa wa Geita iliyoeleza uwepo wa walengwa wasio na sifa kwenye mpango na akawataka wakuu wa mikoa na waratibu wa Tasaf kusitisha malipo pindi tu wanapombaini mnufaika aliyeingizwa kimakosa.
Akizungumzia changamoto ya utapeli unaofanywa na ndugu wa wanufaika au watoa huduma za simu (mawakala) kwa wazee wakati wa malipo, Simbachawene aliitaka Tasaf kuangalia namna mpya ya kuwalipa wazee ili kumaliza changamoto hiyo.