Serikali yafafanua hoja nane uwekezaji Bandari

Dar es Salaam.Wakati wingu zito likitanda katika sakata la makubaliano ya Tanzania na Dubai katika ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika uendelezaji wa bandari, Serikali imejitokeza na kujibu hoja za mkataba huo na sababu za kuichagua Kampuni ya Dubai Port World (DPW). Imewataka wananchi kuwa watulivu na kwamba, kila kinachofanyika maslahi ya Taifa yatazingatiwa kuliko kitu kingine.

Mkataba huo wa mashirikiano wenye ibara 31 ulisainiwa Oktoba 25, mwaka jana na Serikali hizo mbili, ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalumu ya kiuchumi, maegesho ya utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.

Miongoni mwa waliojitokeza kuhoji uwekezaji huo ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyeonyesha wasiwasi kwenye baadhi ya maeneo ya mkataba huo, huku pia wasomi na wadau wa masuala ya uwekezaji na uchumi wakitoa maoni tofauti.

Hoja zinazoibuliwa kutoka kwa wakosoaji hao ni pamoja na ukomo wa uwekezaji huo, ugumu wa kujitoa kwenye mkataba endapo kutatokea kutoelewana, huku kampuni ya DP World ikidaiwa kuwa na migogoro na baadhi ya mataifa iliyoingia makubaliano katika mikataba kama hiyo.

Hata hivyo, akijibu hoja hizo jana, alipokuwa akihojiwa na kituo cha Clouds Media, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa alisema ukomo wa mkataba huo ni miezi 12 pekee.

“Mkataba huu hakuna muda wala hatujui kwa sababu kuna maeneo ya ushirikiano mengi, kwa hivyo hatujui atafanyia kazi sehemu gani, ama tutamkodisha ama ataendeleza sehemu gani, yako maeneo Bandari ya Dar es Salaam tunaweza kuzungumza naye tukafikia suala la muda,” alisema Mbossa na kuongeza:

“Miezi hiyo 12 ni muda wa kukamilisha mikataba ya utekelezaji kwa kujadili vigezo na masharti ya pande mbili pamoja na muda wa mikataba ya utekelezaji. Tunaangalia manufaa ya kiuchumi ya mradi yakoje ndio tunatoa muda, lazima ujue kama Taifa utapata nini ndio utaangalia muda wa kumpatia.”

Mbossa alisema kuhusu uhalali wa mkataba huo, Bunge lina mamlaka ya kuukataa kwa kadiri litakavyojadiliana na kuona inavyofaa.

“Katiba inasema Bunge ndio linaridhia, kwa hiyo litaangalia ambacho Serikali imesaini na upande mwingine, basi linaridhia au halitaridhia," alisisitiza.

Kuhusu madai ya kusainiwa mkataba huo na kuanza kazi kabla ya kuridhiwa, Mbossa alieleza kuwa baada ya Bunge kuridhia kutakuwa na mikataba ya utekelezaji wa shughuli husika kwa kuzingatia sheria, ikiwamo mikataba ya Tehama, mafunzo, uendeshaji na uendelezaji.

Kuhusu hofu ya kuuzwa Bandari ya Dar es Salaam, Mbossa alisema kinachofanyika ni mwekezaji kuongeza ufanisi wa huduma kwa utaratibu wa kukodisha eneo la kufanyia shughuli hizo za kibandari kwa ukomo wa muda utakaowekwa kimkataba kama ilivyokuwa miaka 22 ya mwekezaji TICTS.

Hoja ya tano iliyojibiwa inahusisha madai ya mkataba huo kutokutoa nafasi ya kuvunja mkataba huo kwa nchi moja kati ya hizo zilizosaini mkataba, lakini Mbossa alipinga akisema nchi moja inaweza kuvunja mkataba huo kwa sababu za msingi zitakazotolewa, isipokuwa sababu zisizokuwa za msingi.

Kuhusu madai ya usiri katika hatua za uwekezaji huo kama ilivyoelezwa na Mbowe, Mbossa akisisitiza uwazi uliowekwa na Serikali uliowezesha kuwasilisha bungeni suala hilo, ili kuridhia au kukataa.

“Si kila nchi inaweza kunufaika na uwazi huu wa kufahamu kuna vitu gani vinaendelea. Hii ndio sababu Bunge linajadili,” alisema.
Kuhusu hoja ya kutohusisha uwekezaji huo na upande wa Zanzibar, Mbossa alisema masuala ya Bandari hayahusiki kwenye Muungano na badala yake TPA inahusika na upande wa Tanzania Bara pekee.
 

Kuhusu DP World

Mbossa pia alieleza hatua zilizochukuliwa kabla ya Serikali kusaini mkataba, ikiwamo kuongeza ufanisi wa huduma za Bandari ya Dar es Salaam, ili kuimarisha ushindani wa huduma za kibandari.

Uwezo, uzoefu na mtandao wa kampuni hiyo ya kimataifa ya huduma za bandari, DPW.
Mbossa alisema kampuni hiyo ina uwezo wa kusaidia kuongeza ufanisi wa huduma za meli, shehena katika Bandari ya Dar es Salaam inayohudumia wastani wa meli 12, huku 20 zikisubiri kwa gharama zinazolipwa na wafanyabiashara wa mizigo, tofauti na ufanisi wa Bandari ya Mombasa.

“DP World ana bandari kavu kubwa Kigali ambako mzigo mkubwa unatoka DR Congo, je, ukimwacha akachukua bandari ya Kenya? Na Kenya wametangaza na wenyewe wanakwenda kwenye utaratibu kama wa kwetu kwa hiyo tutashirikiana baadhi ya vitu,” alisema Mbossa.

Alisema kampuni hiyo ikienda Mombasa itaathiri mnyororo wote wa shughuli za kiuchumi katika huduma za usafirishaji wa mizigo inayotoka Kigali na DR Congo.
“Jambo lingine tunazingatia mwenye uhusiano mzuri na kampuni za meli, uzoefu wa kutoa huduma nyingi Afrika.”

Mbali na Mbossa, mbunge wa zamani Shinyanga mjini na Makamu wa kwanza wa Rais katika Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele alitoa maelezo yake akitaka wananchi waiamini Serikali.

“Ninaamini viongozi wa Taifa letu na watendaji wametafakari vya kutosha, kuchambua kikamilifu na kufanya uamuzi kwa maslahi mapana ya nchi,” alisema Masele.
Katika hatua nyingine, Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amelitaka Bunge kujadili suala hilo na kuwaondoa hofu wananchi kuhusu yale yanayojadiliwa mitandaoni.

Kupitia taarifa iliyotolewa na chama hicho jana, Zitto aliwataka wabunge kujadili maeneo yanayowatia hofu wananchi, ikiwemo suala la muda wa mkataba pamoja na vipindi vya kufanya marejeo, kuuzwa kwa bandari na maeneo ya makubaliano sambamba na kuvunjwa kwa mkataba pale pande mbili zikishindwana.

“Suala la umiliki wa kampuni ya uendeshaji kama itakuwa na hisa sawa kwa sawa kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai.

“Pia, suala la ulinzi wa bandari kama vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania pekee ndiyo vitatoa ulinzi,” alisema Zitto, akiwaasa viongozi kulichukulia suala hilo kwa umakini na kuacha kuingiza hisia za kibaguzi.

Kwa upande mwingine, mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dodoma kuwa uwezo wa Tanzania kuendesha bandari ni mdogo, hivyo wanahitajika wawekezaji katika kufanikisha jambo hilo.

“Ndio maana uwekezaji tunaotaka tuuwekeze ni sawasawa na mtu anayemiliki lori, lakini limeharibika halina tairi na kila kitu, sasa anakuja mtu anakwambia ananunua kila kitu ili kijana wako apate kazi na tugawane kitakachopatikana, unapinga?” alihoji mbunge huyo.
 

TLS kuuchambua mkataba

Wakati mjadala huo ukiendelea, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeteua kamati ya wataalamu itakayofanya uchambuzi wa mkataba huo na kisha kuwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Uongozi Juni 12, mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa jana na Rais wa TLS, Harold Sungusia kwa vyombo vya habari ilieleza makamu mwenyekiti wa chama hicho, Aisha Sinda ataongoza timu hiyo kama mwenyekiti.

Kiongozi huyo atafuatiwa na makamu mwenyekiti wake, Dk Hawa Sinare, huku wajumbe wakiwa ni wakili Mpale Mpoki, wakili Stephen Mwakibolwa na wakili Mackphason Mshana.
 

Bunge kuridhia kesho

Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema jana kuwa azimio la Bunge kuhusu kuridhia ushirikiano wa uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa bandari Tanzania, litawasilishwa bungeni kesho kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na wabunge.

Azimio hilo ni mapendekezo ya kuridhia makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa bandari Tanzania la 2023.

Alisema azimio hilo bado liko katika kamati ya pamoja ya Bunge inayojumuisha Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) na Miundombinu ambayo bado inaendelea kupokea maoni ya wadau ambao hawakuweza kufika Juni 6, 2023.

“Azimio sasa bado liko katika ngazi ya kamati ya pamoja kwa mujibu wa kanuni na baada ya kamati kumaliza kazi yake azimio hilo limepangwa kuingia bungeni Juni 10, 2023 kwa ajili ya mjadala na kupitishwa na Bunge,” alisema.

Nyongeza Sharon Sauwa na Ramadhan Hassan.