Serikali yafungua milango soko huru Afrika

Serikali yafungua milango soko huru Afrika

Dodoma. Tanzania imefungua milango kwenye soko la Afrika na mwaka huu itawasilisha bungeni muswada wa kuridhia mkataba wa Eneo huru la biashara la Afrika (CFTA).

Eneo la Afrika lina nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika, idadi ya watu zaidi ya 1.2 bilioni na pato la jumla la dola 3.4 trilioni za Marekani.

Hayo yalisemwa jana Bernard Haule, kaimu mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za uzalishaji kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipofanya mahojiano maalumu na gazeti hili.

Haule alikuwa anazungumzia namna Watanzania watakavyonufaika na mkataba wa eneo huru la biashara la Afrika ambao Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoutia saini jijini Kigali, Rwanda mwaka 2018.

Alisema mkataba huo ili uanze kufanya kazi ilitakiwa kuwa na nchi 22, lakini hadi Desemba mwaka jana nchi 34 zilikuwa zimetia saini.

Kuhusu kuridhiwa, alisema kwa Tanzania kuna utaratibu wa kuridhiwa na Bunge wakati katika nchi zingine Baraza la Mawaziri ndio lenye jukumu hilo.

Alisema mwaka jana Tanzania ilikuwa kwenye uchaguzi mkuu, hivyo haikuwa rahisi muswada huo kupelekwa bungeni, lakini mwaka huu utawasilishwa.


Manufaa kwa Watanzania

Haule alisema CFTA ina manufaa mengi kwa Watanzania, mfano ajira kwa vijana ambao kama watachangamkia soko hilo wataweza kuondokana na tatizo hilo.

“Kama unavyojua sasa hivi tunao wasomi wengi kuanzia vyuo vikuu hadi vyuo vya Veta na ajira ni tatizo la dunia, lakini CFTA inalenga kupanua ajira kuwezesha Watanzania na vijana wa Afrika kupata ajira.

“Kwa Tanzania tunaamini tutakapokua tumeanza kuwa sehemu ya soko hili, Watanzania na hasa vijana na watakuwa wanajua fursa zinazopatikana katika soko hili.

“Tanzania tuna bahati, tunayo maeneo mengi ambayo vijana wetu wanaweza wakashiriki kwa mfano, tukichukua eneo la kilimo na ufugaji, nchi za Afrika zilizo nyingi zinahitaji sana bidhaa kutoka Tanzania.

“Kama unavyojua Tanzania inazalisha mazao mengi ya chakula, kama unavyojua katika nchi nyingi za Afrika haiwezi kupita miaka miwili au mitatu bila kukumbwa na njaa katika moja ya nchi za Afrika.

“Kwa mfano katika miaka iliyopita Tanzania ilitoa chakula cha msaada kwa nchi kama Zimbabwe na nchi zingine. Hii itawezesha watu wawe na uwanja mpana zaidi wa kuuza mazao yao.

Mfano wa mazao yanayohitaji soko ni parachichi, wanafuga na kuna wanaolima mazao mahindi, mtama na mengineyo .

“Tunaamini Tanzania bado inaweza kuwa kapu la chakula la Afrika,” alisema.