Serikali yajibu hoja 5 Loliondo, Ngorongoro

Muktasari:

Serikali ilitumia zaidi ya saa tatu kujibu hoja takriban tano zilizoibuliwa na wanaharakati nchini kuhusu sakata la Loliondo na Ngorongoro huku ikiwaomba mabalozi na wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kimataifa kuamini taarifa inazozitoa.



Dar es Salaam. Serikali ilitumia zaidi ya saa tatu kujibu hoja takriban tano zilizoibuliwa na wanaharakati nchini kuhusu sakata la Loliondo na Ngorongoro huku ikiwaomba mabalozi na wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kimataifa kuamini taarifa inazozitoa.

Serikali imekutana na mabalozi hao baada ya makundi ya wanaharakati na wanasiasa kulalamika juu ya uamuzi wake wa kumega kilometa za mraba 1,500 za ardhi kwa ajili ya kutunza eneo la pori tengefu Loliondo katika Wilaya ya Ngorongoro.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na mabalozi hao jana Dar es Salaam, alisema Serikali inayo dhamira njema katika mpango huo na inazingatia haki za binadamu katika hatua za kuwahamisha, tofauti na taarifa zinazoelezwa na kundi linalopinga mchakato huo.

Kufuatia hatua ya Serikali kuweka amipaka ya eneo hilo, kumeibuka madai ya vurugu wakati wananchi wanapinga hatua hiyo hali iliyosaabisha askari mmoja kuuawa na watu kudhaa kujeruhiwa.

Miongoni mwa madai hayo ni kuwa Serikali inatumia nguvu kuwahamisha wakazi hao ambao ni wazawa na ukiukaji wa haki za binadamu.

Tayari watu 20 wakiwemo viongozi wa vijini na kata kadhaa za Loliondo wamefikishwa mahakamani jijini Arusha wakishtakiwa kwa kosa la mauaji ya askari aliyepigwa mchale.

Katika wasilisho lake lililoelezea historia ya eneo hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori nchini, Dk Maurus Msuha aliwaambia mabalozi hao kwamba hakuna mkazi aliyelazimishwa kuondoka, Ngorongoro.

Alisema tayari kaya 20 zenye wakazi 111 zimeshahamia Kijiji cha Msomera kilichopo Handeni mkoani Tanga kwa hiari.

Idadi hiyo ya walioondoka ni kati ya kaya 290 zilizokuwa zimejiandikisha huku akidai kuna kundi lingine limeridhia kuhamia eneo hilo wiki hii.

Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja alijibu hoja ya muda wa uamuzi, akisema mchakato wa kutenga eneo hilo ulianza mwaka 2008 na uamuzi ulipangwa kutekelezwa mwaka 2013 lakini ilisogeza mbele muda wa utekelezaji wake.

“Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) anatekeleza mpango uliokuwepo mezani,” alisema Masanja akifafanua kuwa lengo la Serikali ni kunusuru maisha ya wakazi hao waliokuwa wakiishi kwenye mazingira hatarishi, ikiwa ni pamoja na kushambuliwa na wengine kuuawa na wanyama wakali.

Kuhusu suala la uasili, Masanja alisema wanaosema eneo hilo ni asili ya Wamaasai wanapotosha, kwa kuwa asili ya wakazi wa eneo hilo ni jamii ya Wahadzabe, ambao walianza kuishi hapo miaka 3,000 kabla ya Kristo wakifuatiwa na jamii ya Datoga miaka 400 kabla ya Kristo kabla ya kuingia jamii ya Wamaasai miaka 250 kabla ya Kristo.

Pia, alisisitiza kuwa hali ya Loliondo ni shwari na uwekeji wa mipaka katika eneo la kilometa 1,500 kwa ajili ya eneo nyeti la mazalia ya wanyama, chanzo cha maji na mapito ya wanyama kwenye eneo hilo umekamilika.

Kuhusu hoja ya umiliki wa ardhi, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alisema kikatiba hakuna Mtanzania mwenye umiliki wa ardhi ila Rais ndiye msimamizi wa ardhi kwa niaba ya wananchi.

“Hatuna ardhi binafsi, hatuna ardhi ya Wasukuma, ardhi ya Wamaasai,” alisema.

“Tulimpoteza askari polisi,” alisema Dk Mdumbaro akiwataka washiriki wa mkutano huo kusimama kwa sekunde chache kuomboleza kifo hicho.

Mgogoro huo uliibuka tena kati ya mwaka 2010 hadi 2016 baada ya kutolewa taarifa na wahifadhi kuwa eneo hilo la kilomita za mraba 1,500 linaendelea kuharibika kutokana na ongezeko la shughuli za ufugaji na za kijamii.

Hata hivyo, Msuha jana alisema changamoto ya eneo hilo ni ongezeko la idadi ya watu kutoka 8,000 mwaka 1959 hadi 110,000 mwaka jana na idadi ya mifugo kutoka 261,889 hadi 1,074,000 katika kipindi hicho.