Serikali yakataa ombi la Katibu Mkuu CWT

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (CWT), Japhet Maganga.

Muktasari:

  • Wakati Katibu wa Mkuu wa Chama cha Walimu (CWT) akiomba kibali cha kuazimwa kwa mara ya tatu na chama hicho, Serikali imemtaka kurejea katika kituo chake cha kazi Wilayani Temeke Oktoba Mosi, mwaka huu.

Dodoma. Serikali imekataa ombi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (CWT), Japhet Maganga la kuendelea kuazimwa na chama hicho na kumtaka kurejea kazini.

Januari 25 mwaka 2023, Maganga na Rais wa CWT, Leah Ulaya waliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa wilaya lakini hawakwenda kuapa.

Leah aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita wakati Maganga akiteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.

Kutakiwa kurejea katika kituo chake cha kazi kumeelezwa kwenye tangazo kwa umma lililotolewa leo Jumamosi Septemba 23, 2023 na mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke.

Katika tangazo hilo, inaonyesha Maganga aliomba kibali cha kuazimwa CWT kwa mara ya kwanza Agosti 2017 kilichomalizika Septemba 30, 2020.

Aliomba nyongeza ya kibali cha kuazima Juni Mosi mwaka 2020 na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi alimpa nyongeza Agosti 10 mwaka 2020 kinachoishia Septemba 30, 2023.

Tangazo hilo linasema Maganga aliomba tena kibali cha kuazimwa kwa mara ya tatu lakini katibu mkuu utumishi hajaridhia maombi hayo.

“Hivyo basi mwalimu Japheth Maganga anapaswa  kurejea kwenye kituo chake cha kazi mara moja Oktoba Mosi,2023,” linaeleza tangazo hilo.

Maganga alichaguliwa kuwa katibu mkuu Desemba mwaka jana na mkutano mkuu wa CWT akichukua nafasi ya Deus Seif aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho.

Hata hivyo, Deus na aliyekuwa mweka hazina wa chama hicho,  Abubakar Alawi walifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma akiomba mahakama ichukue hatua kwa uongozi wa CWT kwa kukiuka amri halali ya mahakama ya kuzuia mkutano mkuu uliomchagua Maganga kufanyika.