Uteuzi wakuu wa wilaya ulivyomaliza ugomvi Chama cha Walimu

Kàtibu Mkuu wa CWT, Japheth Maganga ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa

Muktasari:

Uteuzi wa wakuu wa wilaya wapya umekiacha bila uongozi wa juu Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na sasa kitapaswa kujipanga upya.

Dodoma. Uteuzi wa wakuu wapya wa wilaya umekiacha bila uongozi wa juu Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na sasa kitapaswa kujipanga upya.

Leo Jumatano Januari 25, 2023 Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus ametangaza majina 37 ya wakuu wapya wa wilaya ambao wameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Miongoni mwao wapo Leah Ulaya, rais wa CWT anayekwenda kuwa mkuu wa Wilaya ya Mbogwe.

Vilevile, makamu wa Rais wa CWT, Dinah Mathamani ambaye mkutano mkuu uliazimia kumfukuza ameteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Uvinza huku Katibu mkuu wa chama hicho, Japheth Maganga akiteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Kyerwa.

Ndani ya CWT hakukuwa na utulivu tangu 2021 baada ya rais wake Ulaya kusimamishwa uongozi kabla ya kurudishwa Desemba 16, 2022.

Pia aliyekuwa Katibu Mkuu Deus Seif na Mweka Hazina, Abubakar Allawi walishtakiwa kwa kesi ya jinai na hivyo chama kikabaki mikononi mwa viongozi wa kukaimu.

Mkutano Mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana ulimrejesha katika nafasi yake Ulaya lakini siku hiyo ukamuondoa Mathamani ambaye nafasi yake ilitangazwa iko wazi na ikitarajiwa kuizibwa kwenye Mkutano Mkuu wa Machi mwaka huu.

Mmoja wa watumishi wa CWT amesema kwa sasa watalazimika kufanya uchaguzi kwa nafasi zote 5 kwenye Mkutano Mkuu wa Machi.

"Uteuzi wa Rais umemaliza makundi kwa hiyo tunaanza upya. Katiba inasema lazima ateuliwa mtu yeyote kukaimu nafasi ya katibu na mweka hazina ili kuandaa uchaguzi. Sifa Kuu ni lazima awe mwalimu," amesema mtumishi huo kutoka CWT akiomba jina lake lihifadhiwe.

Kama CWT itakwenda kwa mfumo huo, italazimika kuchagua viongozi watano ambao ni Rais, Makamu wake, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Mweka Hazina.