Serikali yapiga ‘stop’ ujenzi vituo vya mafuta

Muktasari:

Kufuatia ongezeko la ujenzi holela wa vituo vya mafuta nchini, Serikali imesitisha ujenzi huo ili kutoa nafasi ya kufanya tathimini ya ujenzi wa vituo hivyo.

Dodoma. Serikali imesitisha utoaji wa vibali vipya vya ujenzi wa vituo vya mafuta na mabadiliko ya matumizi ya ardhi kwa ajili ya vituo vya mafuta kwa muda wa miezi mitatu kuanzia leo.

 Uamuzi huo umetangazwa leo Alhamisi Novemba 10, 2022 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula.

“Lengo ni kutoa nafasi kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wizara zinazohusika na utoaji wa vibali kufanya tathmini ya kina kuhusu ujenzi wa vituo vya mafuta nchini,” amesema.

Aidha, Dk Angeline ameagiza kusitishwa kutolewa kwa vibali vipya vya ujenzi vinavyokiuka mipango kabambe ya majiji, manispaa, miji na kusitisha ugawaji wa viwanja kiholela unaosababisha taswira za miji kuharibika.

Ametoa mfano wa eneo lililopangwa kuendeleza ujenzi wa maghorofa vibali vifuate mpango.