Serikali yapokea boti ya doria kuimarisha ulinzi baharini

Boti ya doria iliyozinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  kwenye Bandari ya Dar es Salaam leo Jumapili Aprili 21, 2024. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Muktasari:

  • Itatumika kudhibiti uvuvi haramu na upitishaji dawa za kulevya.

Dar es Salaam. Serikali imepokea boti ya doria kuimarisha ulinzi maeneo ya baharini na maziwa makuu kukabiliana na vitendo vya kihalifu majini.

Boti hiyo imenunuliwa na Chuo cha Mipango kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Serikali ya Japan.

Akizungumza wakati wa makabidhiano na uzinduzi wa boti hiyo leo Aprili 21, 2024 katika Bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema itaenda kudhibiti uhalifu, ukiwemo uvamizi ili Watanzania wawe huru katika kutekeleza majukumu yao.

Amesema boti hiyo itatumiaka kutatua changamoto za kunyang’anywa samaki na kupitisha dawa za kulevya, hivyo kudhibiti uhalifu. 

“Tunataka tuongeze uchumi wa mtu mmoja mmoja, hivyo wizara husika zikae chini ziweke mpango wa pamoja wa kuwakamata wale wote wanaoleta matatizo kwa watu wetu,” amesema.

Amesema wakifanya kama timu, wavuvi haramu na wasafirisha dawa za kulevya watadhibitiwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema boti hiyo ina manufaa kwa kukabiliana na magendo kwenye ukanda wa bahari.

“Hali ya magendo bado ipo kwa asilimia si chini ya 40 na inaungwa mkono na baadhi ya watumishi wa umma,” amesema.

Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Shigeki Komatsubara amesema ulinzi wa maeneo ya majini ni chachu ya maendeleo endelevu.

Amesema ulinzi ni jambo la muhimu hivyo anaipongeza Tanzania na UNDP inajivunia katika hili.

Amesema UNDP itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufikia malengo yake ya 2050 na katika maendeleo endelevu. Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa amesema usalama wa baharini unatoa fursa ya kufanya shughuli halali za kiuchumi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema faida zitakazopatikana kutokana na boti hiyo ni kukomesha uvuvi haramu ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya watu wenye nia ovu ya kuharibu rasilimali za nchi.

“Hadi Desemba mwaka 2023 kwa siku moja kulikuwa na milipuko isiyopungua 20. Huu ni uvuvi haramu na uhalifu tumeshawakamata wahusika 24,” amesema.

Mkurugenzi wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Hosea Ngagala amesema wataendelea kuimarisha usimamizi wa boti hiyo ili kufikia malengo ya ulinzi na usalama wa maeneo ya bahari na maziwa makuu.