Serikali yasaini mkataba wa Sh30 bilioni kulinda bahari

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde

Muktasari:

  • Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID) wamesaini hati ya makubaliano ya Sh30 billioni zitakazotumika katika kuilinda bahari, huku wakihakikisha shughuli zote zinazofanyika baharini zinakwenda vizuri.

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha uchumi wa bluu nchini unazidi kukua, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesaini hati ya makubaliano na Shirika la misadaa la Marekani ‘USAID’, ambapo wamepata kiasi cha Dola 13 millioni sawa na Sh30 bilioni itakayotumika katika kuilinda bahari, kwa kuhakikisha shughuli zote za bahari zinakwenda vizuri.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 26, baada ya kumalizika kwa makubaliano hayo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde amesema mradi huo wa ‘Heshimu Bahari’ utakuwa ni wa miaka 5 ambao utakwenda kuisaidia Tanzania katika maendeleo ya uchumi wa bluu. 

“Jambo hili litasaidia kwa kiwango kikubwa sana katika uchumi wa bluu, ambao kwa sasa Tanzania ndio tumekusudia, kuhakikisha moja ya sehemu kubwa ya uchumi wetu utegemewe kutoka uchumi wa bluu” amesema 

Hata hivyo amesema, fedha hizo walizozipata kutoka USAID, zitakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinawafikia wananchi pamoja na kuilinda bahari.

“Sehemu ya fedha hizo kutakuwa na ruzuku kwa wananchi ambazo ni Dola 3 milioni sawa na Sh7.1 billioni ambazo zitajikita katika kuwawezesha wanajamii wanaoishi maeneo yanayoizunguka bahari, ambazo zitawajengea uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali,” amesema.

Ameongeza kwa kusema anaishukuru Serikali ya Marekani kupitia USAID, kwa kuhakikisha wanasaidia kuleta maendeleo nchini Tanzania kwani kwa kufanya hivyo wanaendelea kudumisha uhusiano wao.

Mratibu wa mradi huo wa ‘Heshimu Bahari’ kutoka USAID, Saddick lazier amesema mradi utajikita katika kuimarisha sera zitakazosaidia serikali, sekta binafsi pamoja na jamii kwenye kuimarisha, kuhifadhi, matumizi endelevu ya rasilimaliza bahari.

“Sehemu kubwa ni kushirikiana na sekta binafsi kupitia kwenye mnyororo mzima wa thamani za mazao ya bahari ikiwa ni pamoja na mazao ya mwani, jongoo bahari, kwani kwa tafiti mbalimbali tutatambua maeneo yanayohitaji msadaa,” amesema.

Pamoja na hayo ameeleza kwamba watahakikisha wanawajengea uwezo vikundi vya kina mama pamoja na vijana kwa kuwapatia ruzuku kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za uzalishaji kwa ajili ya maendeleo ya bahari.