Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yataja sababu kukamatwa kina Dk Slaa

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imekanusha taarifa za madai ya kukamatwa Dk Willibrod Slaa, Mpaluka Nyangali maarufu ‘Mdude’ na mwanasheria Boniface Mwabukusi kwa sababu za kupinga utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na  Dubai na badala yake imesema wanatuhumiwa kujihusisha na uhalifu.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatano Agosti 16, 2023 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye imemnukuu akisema: “Ukweli ni kwamba hakuna mtu yeyote aliyekamatwa Tanzania wala hatakamatwa kwa kukosoa tu mkataba wa bandari au mradi, mpango au sera yoyote ya Serikali kuhusu jambo hilo.”

“Watu hao walikamatwa na Polisi kwa kutoa vitisho kwa nia ya kutaka kufanya ghasia kwa lengo la kuipindua Serikali iliyoko madarakani. Baadhi ya watuhumiwa hao walitamka hadharani wakihamasisha wananchi kubeba silaha dhidi ya Jeshi la Polisi Tanzania,” imesema taarifa hiyo.

Nape ameongeza kusema: “Hawa walinaswa ili kutuma ujumbe mzito wa kuwazuia wahalifu kufanya makosa ya jinai. Hata hivyo, Kukamatwa kwao kwa vyovyote vile, hakuzuii uhuru wa mtu kujieleza kwa nchini Tanzania.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu hao wamekamatwa kama sehemu ya utekelezaji wa sheria ili kuzuia machafuko ya kijamii yanayoweza kutokea kutokana na wito wa uasi dhidi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.

Taarifa ya Waziri Nape inakuja huku baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), wakiitaka Serikali kuwaachia bila masharti, yakiamini kukamatwa kwa watatu hao, ni moja ya mbinu za kuwazuia wakosoaji wa Serikali wa mkataba unaohusisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii  kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari (IGA), uliibua mjadala kwa zaidi ya miezi mitatu kabla ya kuhamia kwenye majukwaa ya kisiasa na mahakamani ambako Serikali ilishinda kesi hiyo dhidi ya wanaopinga.

Baada ya kushindwa kesi hiyo, Wakili Mwambukusi aliyeungwa mkono na Mdude alinukuliwa na vyombo vya habari akiahidi kuhamishia harakati hizo nje ya mahakama kabla ya Jeshi la Polisi kuwakamata kwa madai ya kutoa kauli zilizosababisha watatu hao kuhojiwa kwa tuhuma za uhaini.

Mwabukusi aliyekuwa akiongoza jopo la mawakili katika kesi ya kupinga mkataba huo pamoja na Mdude walikamatwa Agosti 11 mkoani Morogoro, saa 8:30 usiku.

“Kauli za kina kuhusu kukamatwa kwa watu hao zimechanganya mambo mawili tofauti: mjadala wa kitaifa unaoendelea kwa uwazi kwa sasa kuhusu mapendekezo ya uwekezaji wa bandari na suala la sheria kwa upande mwingine,”imenukuu taarifa iliyotolewa leo Agosti 16,2023 na Serikali.

Katika ufafanuzi wa taarifa hiyo ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye inafafanua: “Upotoshaji wa makusudi wa habari kuhusu hali halisi katika kukamatwa kwa washukiwa wa uhalifu unatilia shaka nia halisi na uaminifu wa mashirika nyuma ya taarifa hizo.”

Nape anasema miongoni mwa kauli hizo ni pamoja na ile ya Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, akidai imepotosha ukweli kwa nia mbaya kwa kudai kwamba washukiwa walikamatwa "kwa kukosoa tu mpango wa bandari kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)."

“Ukweli ni kwamba hakuna mtu yeyote aliyekamatwa Tanzania wala hatakamatwa kwa kukosoa tu mkataba wa bandari au mradi, mpango au sera yoyote ya Serikali kuhusu jambo hilo.”