Serikali yataja sababu kutoruhusu mbolea kufungwa kwa kilo moja

Naibu Waziri wa Ardhi, Geophrey Pinda akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha 52 cha mkutano wa Bunge la bajeti, jijini Dodoma leo Juni 24, 2024. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Naibu Waziri Geophrey Pinda asema kanuni za mbolea zinahitaji vifungashio maalumu na Serikali itaendelea kudhibiti ubora wa mbolea.
Dodoma. Serikali imesema wazalishaji na waingizaji wa mbolea wanaotaka kufungasha mbolea katika ujazo wa kilo moja wanaruhusiwa kuomba kibali maalumu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Juni 24, 2024 na Naibu Waziri wa Ardhi, Geophrey Pinda kwa niaba ya Waziri wa Kilimo wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Urambo (CCM), Margareth Sitta, aliyehoji kwa nini Serikali isiruhusu mbolea kuwekwa kwenye vifungashio kuanzia kilo moja na zaidi, ili kukidhi mahitaji ya wakulima.
Akijibu swali hilo, Pinda amesema kifungu cha 32 (4) cha Kanuni za Mbolea za Mwaka 2011 kimeainisha kuwa mbolea yabisi (Solid Fertilizers) zitafungashwa kwenye uzito wa kilo 5, 10, 25 na 50.
Pia amesema kifungu cha 32 (5) cha Kanuni hizo kimeainisha kuwa visaidizi vya mbolea (Fertilizer supplements) vitafungashwa katika ujazo wa lita 5, 10, 20, 50 na 100.
Aidha, Pinda amesema kifungu cha 33 (1) kimeainisha kuwa mbolea za kimiminika (Liquid fertilizers) zitafungashwa katika ujazo wa nusu lita (0.5), lita 1, lita 5 na lita 10.
“Kutokana na kuwepo kwa fursa hiyo ya kisheria, wazalishaji/waingizaji wa mbolea wanaotaka kufungasha mbolea katika ujazo wa kilo moja wanaruhusiwa kuomba kibali maalumu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA),” amesema.
Aidha, Pinda amesema Serikali kupitia TFRA inaendelea kudhibiti wafanyabiashara wadogo kupima mbolea katika mizani kama bidhaa za kawaida kwa kuwa kufanya hivyo kunapoteza ubora wa mbolea.
Katika maswali ya nyongeza, Sitta amehoji Serikali inawahakikishiaje mbolea ya tumbaku itafika kabla ya Julai, ili wakulima waanze kutengeneza mashamba yao kwa wakati.
“Je, Serikali iko tayari kupeleka mbolea ya ruzuku karibu na wakulima, ili wasifuate kwa muda mrefu kuchukua mbolea hiyo,” amehoji.
Akijibu swali hilo, Pinda amesema mbolea itafika kwa wakati kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kuanza matayarisho ya awali.
Naye Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM) Francis Ndulane amehoji ni lini Serikali itahamasisha kilimo kinachotumia mbolea katika Wilaya ya Kilwa, ili kukabiliana na changamoto ya kilimo cha kuhamahama kinachosababisha uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Akijibu swali hilo, Pinda amesema kampeni za kilimo cha mbolea kinakwenda kwa nchi nzima na kuwaomba wabunge kuhamasisha.
“Unajua watu wengine wanalima kwa imani kuwa akitumia mbolea anapoteza ardhi ya asili, niwaombe tuungane wote kuwapa hamasa wakulima, ili watambue umuhimu wa mbolea,” amesema.
Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda amesema kuwa mbolea zilizopo katika vifungashio vya kilo chache hazipatikani madukani na kuhoji ni lini Serikali itaviamrisha viwanda na wafunganishaji mbolea hizo kupatikana madukani.
Akijibu swali hilo, Pinda ametoa agizo kwa viwanda vyote vya mbolea kuhakikisha mbolea zilizofungwa kwa kilo chache ambazo zimetajwa kisheria zinapatikana madukani, ili wakulima wazinunue.