Serikali yataka kuongezwa kwa elimu ya chakula na lishe

Thursday October 14 2021
By Fina Lyimo

Hai. Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Nyamizi Bundala amesema wananchi wengi hawana uelewa sahihi wa matumizi ya vyakula bora, hali inayosababisha kukithiri kwa kushamiri kwa magonjwa ya utapiamlo.

Akizungumza leo Oktoba 14, 2021 katika kijiji cha Usari wilayani Hai mkoani hapa ambako kumefanyika Siku ya Afya na Lishe kwa kufanya maonesho maalum la vyakula vya asili na virutubisho, Dk Bundala amesema ukosefu wa elimu ya lishe ni changamoto kwa jamii.

Amesema wananchi wamekuwa wakizalisha vyakula vyenye lishe na virutubisho lakini hawali kwa mpangilio kutokana na kukosekana kwa elimu sahihi ya ulaji wa vyakula mchanganyiko venye lishe sahihi.

 “Ni vyema maafisa afya ngazi za vijiji kutumia mikutano vya hadhara katika vijiji kutoa elimu sahihi juu ya viwango vya matumizi bora ya vyakula ili wananchi waweze kula mlo kamili kwa afya zao bora,” amesema.

Aidha amesema takwimu zinaonyesha mikoa ambayo ndio inazalisha vyakula vingi na vyenye virutubisho ndio inayokabiliwa na utapiamlo na kwamba hali hiyo inatokana na kukosekana kwa elimu sahihi ya matumizi ya vyakula pamoja ni viwango vinavyotakiwa katika ulaji.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu mkoa huo, Gradianus Mgimba amesema maonyesho ya vyakula kama hayo yatasaidia wananchi wa Kilimanjaro kutambua matumizi sahihi ya vyakula lishe.

Advertisement

“Maonyesho ya siku ya lishe yanaenda  sambamba na wiki ya maadhimisho ya siku ya chakula duniani iliyozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,  Stephen Kagaigai Oktoba 12, 2021 na  kilele chake kitafanyika Oktoba 17 katika viwanja vya Mandela Pasua mjini Moshi,” amesema.

Naye ofisa mtendaji wa Kata ya Machame Narumu Merystela Shirima amesema wahudumu wa afya ngazi ya jamii wametakiwa kuelimisha wananchi namna ya kutambua dalili za utapiamlo na jinsi ya kuziepuka.

Advertisement