Seven aeleza majukumu yake Sony Music

Wednesday December 16 2020
sevenpic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Christine Mosha maarufu Seven ambaye alikuwa  meneja wa mwanamuziki Alikiba, ameteuliwa kuwa meneja wa masoko na wasanii wa kampuni kubwa ya muziki duniani ya Sony Music kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

Seven anakuwa wa kwanza kushikilia nafasi hiyo kwani awali kampuni ya Sony haikuwa na mwakilishi kwa ukanda huo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Desemba 16, 2020, Seven ameelezea majukumu yake katika nafasi hiyo ni  kutafuta wasanii wapya na kuwasajili, kukuza muziki wa Afrika Mashariki na kuingiza katika soko la dunia.

"Sehemu ya majukumu yangu itakuwa ni kusajili wasanii wapya na kuendelea kuwakuza wasanii wa Afrika Mashariki ambao wanafanya kazi chini ya Sony na  kuhakikisha  sound ya Afrika Mashariki inakwenda kwenye soko la dunia." Ameeleza Mosha.

Huku akizungumza kwa furaha amesema, “biashara ya burudani ina changamoto nyingi kwa wanawake, lakini kutokana na uzoefu nilionao nina uhakika tutafanikiwa kwa pamoja kama Afrika Mashariki na kufika mbali."

 Amebainisha kuwa kwa sasa kampuni hiyo ina wasanii watatu wa Afrika Mashariki inayofanya nao kazi akiwemo Ommy Dimpoz kutoka Tanzania.

Advertisement
Advertisement