Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh11.6 bilioni kuboresha huduma ya maji Wilaya ya Kishapu

Naibu Katibu Wizara ya Maji, Cyprian Luhemeja (aliyevaa kofia na miwani ya kukinga mwanga wa jua) akisisitiza jambo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji wilayani Kishapu. Kushoto kwake ni Mbunge wa Kishapu, Boniphace Butondo. Picha na Suzy Butondo.

Muktasari:

Miradi hiyo mitatu inayotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh11.6 bilioni itawapunguzia wananchi adha ya kutembea umbali mrefu na kutumia fedha nyingi kupata huduma ya maji.

Shinyanga. Zaidi ya wananchi 78,233 kutoka Kata za Lagana, Ndoleleji Masanga na Seseko Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamepata matumaini ya kuondokana na tatizo la ukosefu wa majisafi na salama baada ya Serikali kuanza kutekeleza miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya Sh11.6 bilioni katika maeneo yao.

Miradi hiyo iliyotembelewa na kukaguliwa na Naibu Katibu Wizara ya Maji, Cyprian Luhemeja aliyetembelea Mkoa wa Shinyanga Julai 20, 2023 ni ile ya Kata ya Lagana inakojengwa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita za ujazo 90, 000 itakayohudumia zaidi ya watu 49, 000 inayotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh6.6 bilioni.

Serikali pia inatekeleza mradi wa maji wa maji Kata ya Seseko kwa gharama ya zaidi ya Sh 2.7 bilioni itakayohudumia zaidi ya watu 15, 000. Mradi huo pia unahusisha ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita za ujazo 100,000.

Katika ziara yake hiyo, Naibu Katibu mkuu huyo pia amekagua mradi wa maji unaotekelezwa katika Kata za Masanga na Ndoleleji kwa gharama ya zaidi ya Sh 2.3 bilioni inayohusisha ujenzi wa miundombinu ikiwemo matenki mawili yatakayohifadhi lita 100,000. Mradi huo utahudumia zaidi ya watu 12,768.

Akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali na taasisi zake wilayani Kishapu, Luhemeja ameelezea kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo huku akiwahimiza makandarasi kuhakikisha inakamilika kwa wakati uliopangwa.

‘’Wananchi wote wanaotaka huduma waunganishiwe kwa wakati. Lengo la Serikali ni kumtwaa mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha huduma ya maji inapatikana umbali usiozidi mita 400,’’ amesema Luhemeja

Meneja wa (Ruwasa) Wilaya ya Kishapu, Dicksoni Kamazima amesema hadi sasa, huduma ya maji wilayani humo unapatikana kwa asilimia 56 huku jitihada zikiendelea kuhakikisha kiwango hicho kinafika asilimia 90 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Akizungumzia upatikanaji na maboresho ya huduma ya maji mkoani Shinyanga, Meneja wa Ruwasa mkoani humo, Julieth Payovela amesema mkoa huo unatarajiwa kupokea zaidi ya Sh28.9 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji mkoani humo kwa mwaka wa fedha wa 2023/24.

Wananchi watoa ya rohoni

Charles Ndungulu, mkazi wa Kijiji cha Lagana licha ya kuipongeza Serikali kwa kutekeleza miradi hiyo, ameziomba mamlaka husika kuhakikisha utekelezaji unafanyika na kukamilika kwa ubora na kwa muda uliopangwa.

‘’Miradi hii ni ukombozi kwetu kwa sababu itatupunguzia adha ya kutembea umbali kilometa 14 kutafuta huduma ya maji, na gharama kubwa ya kati ya Sh500 hadi Sh700 ya kununua ndoo au dumu la maji lenye ujazo wa lita 20,’’ amesema Ndunguru

Kauli hiyo imeungwa mkono na Mariam Jilala, mkazi wa Kijiji Cha Ndoleleji akisema huduma ya uhakika ya maji itaimarisha maisha na afya za wananchi kwa kupunguza maradhi yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo salama.

‘’Tatizo la maji ilichochea hata migogoro kwenye baadhi ya familia kwa wanawake kutumia muda mrefu kutafuta maji kiasi cha kuibua hisia ya wivu kutoka kwa wanaume wakihisi pengine wamepitia kwingine,’’ amesema Mariam

Mtendaji wa Kijiji cha Shokashoka, Ally Lugito ameiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo kuwezesha wananchi kupata huduma karibu na hivyo kutumia muda wao mwingi kwenye shughuli za uzalishaji mali.

Mbunge wa Kishapu, Boniphace Butondo ameiomba Serikali kuongeze fedha za kutekeleza miradi ya maji katika vijiji ambavyo ama vinavyopitiwa au jirani na bomba la mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria.

‘’Bomba kubwa la maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mikoa ya Tabora na Dodoma lazima iwanufaishe wananchi kwenye vijiji ambako bomba linapita,’’ amesema Butondo

Mkurugenzi mtendaji wa wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga/Kahama, Patrick Nzamba amesema mamlaka hiyo inaendelea kutafuta vyanzo vingine vya maji ikiwemo kuchimba visima na mabwawa kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kufikia asilimia 85 hadi 95 maeneo ya vijijini na mijini.