Sh2 bilioni zajenga jengo la huduma ya macho Bugando

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la CBM Tanzania, Nesia Mahenge (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Muktasari:
Shirika la Maendeleo duniani la Christian Blind Mission (CBM) limetumia zaidi ya Sh2 bilioni kujenga jengo la huduma ya macho katika hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza
Arusha. Shirika la Maendeleo duniani la Christian Blind Mission (CBM) limetumia zaidi ya Sh2 bilioni kujenga jengo la huduma ya macho katika hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Ijumaa Aprili 8 , 2022 Mkurugenzi Mkazi wa Shirika hilo nchini Tanzania, Nesia Mahenge amesema kuwa mradi huo umechukua mwaka mmoja na unalenga kuwasogezea karibu huduma wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa kupata matibabu ya macho.
Amesema kuwa, Shirika hilo kwa kushirikiana na Serikali, hospitali ya Bugando na wadau mbalimbali limefanikiwa kukamilisha jengo hilo kwa asilimia 95 ambalo litasaidia kutoa huduma ya macho na walemavu kwa kanda ya ziwa lengo likiwa ni kutokomeza magonjwa ya macho na upofu nchini.
"Hospitali ya macho tunayoijenga hapa Bugando imekamilika kwa asilimia 95 na itakuwa mkombozi kwa wakazi wa mikoa ya ziwa lengo ni kuhakikisha tunapunguza magonjwa ya macho hapa Tanzania "amesema.
Amesema kuwa, Shirika la CBM Tanzania limekuwepo hapa nchini kwa takribani miaka 50 na limekuwa likisaidia kutoa huduma jumuishi ya afya ya macho kwa watoto na wenye ulemavu, watu wazima kwa kuzuia upofu na kutibu uoni hafifu.
Amesema kuwa, mkutano unaoendelea jijini Arusha unalenga kuangalia ukubwa wa changamoto ya afya ya macho hapa nchini, baada ya kutambua kuwa asilimia 80 ya magonjwa ya macho yanatibika na hivyo kuangalia namna ya kuongeza nguvu ili kutatua changamoto za macho.
"Tuna mpango wa kuongeza huduma ya macho ili kupunguza changamoto kwa wakazi wa kanda ya kaskazini ambao wamekuwa wakifuata huduma ya macho umbali mrefu katika hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro "amesema.
Mkurugenzi wa miradi ya Afrika Mashariki na Kusini, Albert Kombo kutoka nchini Kenya amesema nchi ya Tanzania ni kati ya nchi tisa wanazotekeleza miradi ya huduma ya afya ya macho duniani.
Amesema kuwa,tangu shirika lao liendeshe shughuli zake hapa nchini wamepata ushirikiano mzuri na serikali na kuahidi kupanua huduma zaidi ya miradi ya afya ya macho na ulemavu nchini.