Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh45.9 bilioni kujenga miundombinu Chuo Kikuu cha Julius Nyerere

Baadhi ya viongozi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) na wawakilishi makandarasi wakiangalia ramani ya baadhi ya majengo yanayotarajiwa kujengwa katika kampasi Kuu ya Butiama.  Picha na Beldina Nyakeke 

Muktasari:

Tayari Serikali imetoa zaidi ya Sh103 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho yakiwemo majengo 21 yanayotarajiwa kujengwa katika kampasi Kuu ya Butiama na kituo cha Tabora.

Butiama. Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kimesaini mikataba mitatu yenye thamani ya zaidi ya Sh45.9 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujezi wa miundombinu ya chuo hicho, kazi inayotarajiwa kuanza Novemba 27, 2023.

Hafla ya kusaini mikataba hiyo imefanyika mjini Butiama leo Novemba 13, 2023, na hivyo kufikisha idadi ya mikataba ya ujezi wa miundombinu ya chuo hicho kufikia minne baada ya mkataba mwingine wa mshauri mwelekezi kutoka kampuni ya Epitome Architects ya jijini Dar es Salaam wenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni kusainiwa wiki mbili zilizopita.

Mikataba iliyosaniwa leo inahusu ujenzi wa jengo la ghorofa nne la hosteli, Shule ya Kilimo na Shule ya Madini inayotekelezwa kupitia kampuni za za Shandong High Speed Deijan na Jiangxi International Economic and Technical Cooperation, zote kutoka nchini China.

Mkadiriaji Majenzi wa MJNUAT, Oswald Beatus amesema utekelezaji wa miradi ya hosteli na bwalo la chakula unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 15 wakati ujenzi wa Shule za Kilimo na Madini utakamilika ndani ya miezi 18 ijayo.

"Hosteli itakuwa na uwezo wa kulaza wanafunzi 400 kwa wakati mmoja huku bwalo likiwa na uwezo wa kuhudumia watu 500 kwa wakati mmoja," amesema Oswald

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Lesakit Mellau ameahidi kuwa uongozi wa chuo hicho utasimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo kuhakikisha inakuwa na ubora kulingana na thamani halisi ya fedha.

John Nyantika, mkazi a Butiama ameipongeza Serikali kwa kuanza kutekeleza miradi ya ujenzi wa chuo hicho ambacho kwa sasa kinatumia kwa muda majengo ya iliyokuwa shule ya Sekondari ya Oswald Mangómbe.

Amesema uwepo wa chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 2005 siyo tu ni kuenzi na kuendeleza falsafa ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuhusu sekta ya kilimo, ustawi wa watu na maendeleo ya Taifa, bali pia ni fursa ya kukua kiuchumi kwa wakazi wa Wilaya ya Butiama ambako ndiko alikozaliwa mwasisi huyo wa Taifa.

"Kwetu wana Butiama uwepo wa chuo hiki ni zaidi ya kuona Watanzania wakisoma na kubobea katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi, bali pia ni heshima kwa Mwalimu Nyerere na fursa ya kiuchumi kwa wananchi,’’ amesema Nyakitita.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Agatha Jacton akisema; "Ujenzi wa chuo kilimo hapa kwetu ni fursa kwetu kwa sababu tutapata fursa za ajira na biashara ya bidhaa na huduma kuanzia kwa mafundi na wanafunzi,’’

Tayari Serikali imetoa zaidi ya Sh103 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho yakiwemo majengo 21 yanayotarajiwa kujengwa katika kampasi Kuu ya Butiama na kituo cha Tabora.