Sh466 milioni za bilionea Laizer zajenga shule Simanjiro

Sh466 milioni za bilionea Laizer zajenga shule Simanjiro

Muktasari:

Bilionea wa Kitanzania, Saniu Laizer amekamilisha ujenzi wa shule ya Msingi Mkoani Manyara katika Kijiji cha Naepo yenye thamani ya Sh466 milioni.

Simanjiro. Bilionea wa Kitanzania, Saniu Laizer amekamilisha ujenzi wa shule ya Msingi Mkoani Manyara katika Kijiji cha Naepo yenye thamani ya Sh466 milioni.

Laizer amekamilisha ujenzi wa madarasa hayo ikiwa ni miongoni mwa ahadi zake alizotoa baada ya kufanikiwa kupata mawe ya madini ya Tanzanite yenye kilo 15 ikiwa ni thamani ya 7.7 bilioni.

Shule hiyo iliyopewa jina la Saniniu Laizer ina jumla ya madarasa sita na ofisi nne ikiwamo ofisi ya utawala, ofisi ya Mwalimu Mkuu, Mwalimu mkuu msaidizi na ofisi kwa ajili ya mikutano ya shule, ikiwa imetumia ya 466 milioni.

“Shule hii serikali ikiniunga mkono nitakua pamoja nao na kuna majengo ambayo bado sijamaliza ila nitayamalizia, kama ingewezekana hii shule kuwa English Medium mimi nina uwezo hata wa kujenga mabweni ya kulala wanafunzi,” alisema Laizer.

Kwa mujibu wa Laizer, mpaka sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 150 watakaoanza darasa la kwanza na ameikabidhi kwa serikali ili kupata walimu wenye ujuzi.

Wakati akizindua shule hiyo, Katibu Tawala wilaya ya Simanjiro, Zuena Omari kwa niaba ya mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, alimpongeza Laizer kwa fadhila zake kwa wananchi wa Simanjiro.