Sh68 bilioni za Tasaf zatekeleza miradi 353 ya maendeleo Geita

Katibu Tawala mkoa wa Geita Mohamed Gombati akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa miradi ya Tasaf.
Muktasari:
- Mpango wa Tasaf kwa Mkoa wa Geita umewezesha wanafunzi zaidi ya 89,000 kupata mahitaji ya shule na watoto 7,582 walio chini ya miaka mitano kuhudhuria kliniki kwa ajili ya huduma na elimu ya malezi.
Geita. Mkoa wa Geita umepokea zaidi ya Sh68 bilioni kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, fedha ambazo zimesaidia kaya maskini na kutekeleza miradi 353 ya maendeleo kwenye jamii.
Katibu tawala wa mkoa huo, Mohamed Gombati amebainisha hayo leo Mei 26, 2025, katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa miradi ya Tasaf na kati ya fedha hizo, Sh5.3 bilioni ni kwa ajili ya walengwa 37,688 kupitia mpango wa uhawilishaji fedha, na Sh18 bilioni zilitumika kutekeleza miradi ya maendeleo ya kijamii.
Amesema kwa lengo la kukuza uchumi wa kaya, vikundi 1,795 vyenye wanachama 24,643 vimesajiliwa na tayari vimeweka akiba ya zaidi ya Sh509 milioni.
Aidha, Sh592 milioni zimetumika kufanikisha miradi ya ufugaji kupitia vikundi 63 vya wanufaika, huku Sh1.2 bilioni zikielekezwa kwenye ajira za muda kama vile upandaji miti, uchimbaji visima, barabara na ujenzi wa malambo.
“Mkoa pia umeongezewa Sh18 bilioni baada ya kufanya vizuri kwenye utekelezaji wa miradi katika wilaya za Chato na Mbogwe kwa ajili ya miradi ya afya na elimu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kupunguza umaskini,” amesema Gombati.
Hata hivyo, amebainisha changamoto ambapo baadhi ya kaya zenye wazee nguvu kazi inayosajiliwa huhama baada ya muda, jambo linalovuruga utekelezaji wa shughuli za ajira za muda. “Wakati mwingine mzee hulazimika kufanya kazi mwenyewe ili asikose malipo,” ameeleza.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Tasaf, Salome Mwakigomba amesema Geita ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa utekelezaji bora wa miradi ya Tasaf kitaifa, na Halmashauri ya Wilaya ya Chato ikiongoza kati 33.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba akichangia kwenye kikao hicho, amesema Tasaf imechangia kupunguza utoro katika Shule ya Sekondari Izumacheli kwa kujenga mabweni yaliyosaidia wanafunzi kuepuka kutumia mtumbwi kuvuka maji kila siku kwenda na kurudi shule.
Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amewataka waratibu na wakurugenzi kuhakikisha miradi inayosalia inakamilika kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha, Juni 30, 2025, huku akisisitiza umuhimu wa manunuzi kwenda sambamba na malipo ya mafundi ili kazi zikamilike kwa wakati.