Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh9.9 bilioni kusambaza maji vijiji 15 Nyanghwale

Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira vijiji (Ruwasa) wilayani Nyang’hwale, Moses Mwampunga akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji Wilayani humo.

Muktasari:

  • Serikali imetenga Sh9.9 bilioni kwa ajili ya uchimbaji wa visima virefu pamoja na kusambaza miundombinu ya maji, ili kuhakikisha ifikapo 2025 vijiji vyote vya wilaya hiyo vinapata huduma ya maji safi na salama.

Geita. Kati ya vijiji 62 vilivyopo Wilaya ya Nyanghwale, mkoani Geita, vijiji 15 havina huduma ya maji safi na salama.

Kutokana na changamoto hiyo, Serikali imetenga Sh9.9 bilioni kwa ajili ya uchimbaji wa visima virefu na usambazaji wa miundombinu ya maji, ili kuhakikisha vijiji vyote vinapata huduma ya maji safi ifikapo mwaka 2025.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Septemba 18, 2024 na Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) wilayani humo, Moses Mwampunga.

Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha maji safi na salama yanawafikia wananchi wote.

Mwampunga amesema licha ya vijiji 15 kukosa maji, idadi ya vijiji vilivyopata huduma imeongezeka kutoka sita mwaka 2021 hadi 47 mwaka huu.

“Mtandao wa maji umeongezeka pia, kutoka vijiji viwili mwaka 2021 hadi vijiji 39, sawa na asilimia 75 ya vijiji vyenye mtandao wa maji,” amesema.

Mwampunga amesema wanapanga kuchimba kisima katika kila kijiji na kuweka miundombinu ya umeme wa jua, ili kuimarisha upatikanaji wa maji.

Aidha, mpango mwingine ni kupeleka maji kutoka bomba kuu linaloyatoa Ziwa Victoria, ili kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini ifikapo mwaka 2025.

Mkuu wa Wilaya ya Nyanghwale, Grace Kingalame amesema upatikanaji wa maji kwa sasa umefikia asilimia 75, lengo likiwa ni asilimia 85 kama ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inavyoelekeza.

Amesema kwa miaka mitatu iliyopita, Serikali imetoa Sh9.4 bilioni kwa miradi ya maji, ikiwa ni juhudi za kumtua mwanamke ndoo kichwani.

Wakazi wa Nyanghwale, akiwamo Renatha Revocatus amesema hali ya upatikanaji wa maji imeboreshwa, ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Amesema walikuwa wakiamka usiku kutafuta maji, huku wakikabiliana na hatari za wanyama wakali kama fisi na wengineo.

Naye Pendo James, mkazi wa Kharumwa amesema gharama za maji zimepungua kutoka Sh500 kwa ndoo ya lita 20 hadi Sh50.