Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shahidi: Mussa hahusiki mauaji ya bilionea Msuya

Muktasari:

  • Katika tovuti na gazeti letu ana, tulikuletea ushahidi wa shahidi wa nane wa Jamhuri, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Herman Ngurukizi ambaye alisoma maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu akieleza alichokifahamu juu ya mauaji hayo.


Agosti 7, 2023 Jiji la Arusha na miji ya Moshi na Mirerani ilitikiswa na taarifa za kuuawa kwa kupigwa risasi mfanyabiashara maarufu wa madini, Erasto Msuya, maarufu kwa jina la Bilionea Msuya, tukio lililotokea wilayani Hai.

Katika tovuti na gazeti yetu jana, tulikuletea ushahidi wa shahidi wa nane wa Jamhuri, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Herman Ngurukizi ambaye alisoma maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu akieleza alichokifahamu juu ya mauaji hayo.

Mangu katika maelezo hayo alieleza namna laini nne zilivyosajiliwa mahususi kuratibu mawasiliano ya mipango ya mauaji hayo, alivyowapeleka washtakiwa wawili nchini Kenya kununua bunduki ya SMG iliyotumika katika mauaji hayo.

Vilevile tuliishia pale ambapo shahidi huyo aliulizwa maswali ya dodoso na wakili Hudson Ndusyepo aliyekuwa anamtetea mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed. Leo tunaendelea na maswali ya dodoso ya mawakili wengine.

Mahojiano kati ya mawakili hao, Majura Magafu, Emanuel Safari na John Lundu mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo iliyokuwa na mashahidi 27 wa kuongea moja kwa moja kortini yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Magafu: Angalia kielelezo hicho na uonyeshe ni ukurasa gani unaoonyesha kuwa mtuhumiwa amekiri kuwa ameua.

Shahidi: Hakuna ukurasa unaoonyesha hivyo, lakini inaonyesha ushiriki wake na vitu vilivyosababisha Msuya kuuawa.

Wakili Magafu: Utakubaliana na mimi kuwa wakati unaenda kuandika maelezo ulikuwa hujaongea na mtuhumiwa kitu chochote?

Shahidi: Kabla ya kuanza kumhoji sijaongea naye chochote.

Wakili Magafu: Sasa nani alikwambia kuwa mtuhumiwa amehusika na mauaji hayo?

Shahidi: Mimi niliambiwa nikamchukue maelezo Mussa Mangu kuhusiana na tukio la mauaji.

Wakili Magafu: Utakubaliana na mimi kuwa mshtakiwa wa tatu alisema yeye hahusiki katika mauaji kutokana na hiki kielelezo?

Shahidi: Kutokana na mauaji hayo kwa ujumla yeye hakushiriki.

Wakili Magafu: Utakubaliana na mimi unapochukua maelezo ya mtuhumiwa hatakiwi kutoa maoni, bali maelezo yake na hutakiwi kumuuliza swali linalomtaka atoe maoni?

Shahidi: Nimeandika maelezo niliyoambiwa na mtuhumiwa.

Wakili Magafu: Kutokana na maelezo yaliyosomwa, mshtakiwa wa tatu alikuwa anajiondoa katika ushiriki, utakubaliana na mimi?

Shahidi: Mahakama itaamua kutokana na maelezo niliyoandika.

Wakili Magafu: Utakubaliana na mimi mshtakiwa alikataa kubeba mzigo (bunduki) ambao hakuutambua kule Namanga?

Shahidi: Alichosema mshtakiwa ndicho nilichokiandika na si jukumu langu kutafsiri alichokieleza mtuhumiwa.

Wakili Magafu: Mshtakiwa wa tatu alikueleza juu ya ununuzi wa pikipiki, je, aliwahi kukutajia namba za usajili wa pikipiki hizo?

Shahidi: Hapana.

Wakili Magafu: Uliwahi kumuuliza kama Erasto Msuya anayemzungumzia anamfahamu?
Shahidi: Hilo swali sikumuuliza.

Wakili Magafu: Kwa nini hukumuuliza hilo swali ili kujua kama anamfahamu marehemu au vipi?
Shahidi: Swali hilo halikunijia muda huo.

Wakili Magafu: Swali hilo lilikuwa na umuhimu au halikuwa na umuhimu?
Shahidi: Kwangu lilikuwa halina umuhimu.

Wakili Magafu: Kwenye maelezo yanasema, “biashara itafanyika hapa” je, uliwahi kumuuliza kwamba ni biashara gani?

Shahidi: Sikumuuliza.

Wakili Magafu: Uliwahi kumuuliza mtuhumiwa kuwa zile pikipiki zilinunuliwa kwa kusudio gani?
Shahidi: Sikuwahi kumuuliza.

Wakili Magafu: Uliwahi kumuuliza zile laini zilisajiliwa kwa kusudio gani?
Shahidi: Sikumuuliza.

Wakili Safari: Maelezo ya nyongeza ulianza kuandika saa ngapi na kumaliza saa ngapi?
Shahidi: Nilianza kuandika saa nane na kumaliza saa tisa.

Wakili Lundu: Unajua kwamba sentensi ya onyo ni kukiri, ni kweli?

Shahidi: Ukosa sahihi.

Wakili Lundu: Kwa maneno hayo na kielelezo hicho ulichokitoa mahakamani, mshtakiwa alikiri?
Shahidi: Kwa maelezo aliyotoa na kuandika kwangu alikiri.

Wakili Lundu: Je, wakati unachukua maelezo ya nyongeza ulimpa haki yake mtuhumiwa sawa na ulizompa jana yake ulipokabidhiwa na RCO?

Shahidi: Ndiyo nilimpa.

Wakili Lundu: Uliziandika hizo haki zake kwenye maelezo yake?

Shahidi: Nilimpa ila sikuziandika nilimsomea za jana yake.

Kwa upande wake, shahidi wa tisa wa Jamhuri, Inspekta Samwel Maimu kutoka ofisi ya RCO Kilimanjaro, alisema Agosti 7, 2013 saa 6.30 mchana alipokea simu kutoka kwa RCO akimpa taarifa ya mauaji ya Bilionea Msuya na kumtaka aende eneo hilo.

Akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavulla, shahidi huyo alisema alipofika eneo la tukio akiwa na makachero wenzake, walikuta mwili wa marehemu, pembeni kulikuwa na gari lake aina ya Range Rover na alikagua eneo.

“Tulifanikiwa kupata maganda 22 ya risasi eneo la tukio na pia bastola kwenye maungo ya mwili wa marehemu ikiwa na magazine mbili. Pia tulipata simu mbili, moja Samsung na nyingine Iphone. Mwili ulikuwa na majeraha ya risasi,” alisema.

Alichora ramani ya eneo la tukio na kuupeleka mwili hospitali ya Wilaya ya Hai ila akasema wakati anafika eneo hilo alikuwa hafahamu marehemu ni nani.

Alieleza wakiwa bado katika eneo hilo, walipokea taarifa kuwa kuna pikipiki ilikuwa imetelekezwa upande wa Kaskazini wa Orkalili, walielekea huko na kuipata pikipiki hiyo aina ya Toyo, kofia ngumu (helimeti) na nguo aina ya jacket.

Shahidi huyo aliomba mahakama ipokee ramani aliyoichora kama kielelezo, lakini mawakili wa utetezi walipinga kupokewa kwa kielelezo hicho. Mwisho wa siku Jaji Salma Maghimbi alitupilia mbali pingamizi hilo na kuipokea ramani hiyo.

Akiendelea kutoa ushahidi, alisema gari la marehemu walilolikuta eneo la tukio ni aina ya Range Rover namba T800 CKF, akasema kwa wakati huo akiwa kizimbani alikuwa hakumbuki namba zake za chesisi na kuomba ajikumbushe.

Wakili aliiomba mahakama itoe ruhusa ili shahidi huyo aweze kulitambua gari hilo na mahakama ikatoa amri kuwa wadaawa wa kesi hiyo waende nje ya mahakama ili shahidi alitambue, hata hivyo alishindwa kufungua boneti kusoma chesisi.

Baada ya mahakama kurejea, wakili Chavula aliomba gari hilo litolewe kama kielelezo lakini mawakili wa utetezi walipinga wakisema si shahidi sahihi wa kuweza kulitoa na hakueleza mnyororo wa kielelezo hicho.

Katika uamuzi mdogo, Jaji Maghimbi alikubali ombi hilo akisema anakubaliana na hoja ya upande wa utetezi kuwa shahidi alikuwa ametokea Himo na katika ushahidi wake hakueleza siku ya juzi alikuwa amelitoa wapi.

Shahidi huyo alisema baada ya kukusanya vielelezo vyote katika eneo la tukio, walivipeleka Kituo cha Polisi Bomang’ombe na baadaye akavihifadhi ofisi ya RCO kwa ajili ya kuvitunza na yeye wakati huo ndiye alikuwa mtunza vielelezo.

Baada ya kukamilisha hilo, alienda Arusha kuungana na timu ya uchunguzi, akiwa ni mkuu wa timu ya ukamataji.

Alipofika Arusha Agosti 12, 2013, walipewa jina la Mussa Mangu na namba yake kwamba wanatakiwa kumkamata.

“Sikuwa namfahamu Mangu kabla ya siku hiyo. Baada ya kupata namba yake nilimpigia simu akatuambia yuko KIA na tukakubaliana kuonana eneo la King’ori. Baada ya kujitambulisha kwake alikubali kuwa yeye ndio Mussa Mangu.

“Agosti 13,2013 tulitakiwa kumkamata mtu aitwaye Sharifu Mohamed (mshtakiwa wa kwanza). Tulipogonga nyumbani kwake mlinzi wake akatuambia hayupo. Halafu Sharifu alijitokeza, tukamkamata tukamkabidhi Arusha,” alisema.

Shahidi huyo alisema Agosti 18, 2013 walikuwa bado jijini Arusha, ambako timu ya kufuatilia mawasilino (Cyber Team) waliwapa majina mawili, Ally Majeshi (mshitakiwa wa 7) na Jalila Zuberi (mshitakiwa wa nne) kwa ajili ya kuwakamata.

“Tulifika Babati Agosti 18, 2013 tukaambiwa kuwa hao watu wameenda Kijiji cha Kisesadisa huko Kondoa. Tulielekea Kisesadisa ambako tulijulishwa wamepanga katika nyumba ya kulala wageni ambayo haikuwa na jina,” alieleza.

“Kwenye saa nane usiku tulimkamata Jalila na alivyohojiwa alisema hajui lolote na kwamba atatoa maelezo yake mahakamani. Tulipomkamata alikuwa peke yake kwenye chumba. Ally hakuwepo ndani ya kile chumba,” alisema na kuongeza:

“Mhudumu wa ile nyumba akatuambia Ally alikuwa na Jalila lakini aliondoka kwenye hiyo nyumba saa sita usiku huo bila kueleza anaenda wapi. Sikuwa namfahamu hata mmoja wakati naenda kuwakamata watuhumiwa hao.”

Baada ya kumkamata Jalila, walirudi naye Babati na baadaye Arusha na wakati wote wa ukamataji, alikuwa na makachero wenzake aliowataja kuwa ni Koplo Atway, Selemani, Derick na Lameck. Walienda kumkabidhi Jalila jijini Arusha.

Usikose kufuatilia simulizi ya kesi hii ya mauaji ya Bilionea Msuya kesho.