Shahidi wa tano kutoa ushahidi kesi kina Mbowe

Muktasari:

  •  Mahakama Kuu ya Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, leo Alhamisi Novemba 25, 2021 inatarajia kusikiliza ushahidi wa shahidi wa tano katika kesi ndogo ndani ya kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.


Dar es Salaam.  Mahakama Kuu ya Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, leo Alhamisi Novemba 25, 2021 inatarajia kusikiliza ushahidi wa shahidi wa tano katika kesi ndogo ndani ya kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi iliibuka baada ya mshtakiwa wa tatu, Mohamed  Abdillahi Ling'wenya kupinga maelezo ya onyo yaliyotolewa na shahidi wa Jamhuri, SP Jumanne akidai hakuwahi kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam na kwamba alilazimishwa kusaini maelezo ambayo hakuyatoa.

Washtakiwa hao wamekuwa wakidai walihifadhiwa katika Kituo cha Polisi Tazara tangu walipofikishwa Dar es Salaam wakitokea Moshi, Kilimanjaro walikokamatwa kwa tuhuma za kupanga kutekeleza vitendo vya kigaidi.

Tayari mashahidi wanne kati ya sita wanaotarajiwa kutoa ushahidi wameshatoa katika kesi hiyo ndogo na leo shahidi wa tano anatarajiwa kutoa ushahidi.

Jana Jaji Joachim Tiganga aliahirisha kesi hiyo na kusema itaendelea kusikilizwa leo saa 3 asubuhi.

Mwananchi digital itaendelea  kukuletea mwenendo wa kesi hii moja kwa moja kutoka mahakamani hapa kadri kesi itakavyokuwa inaendelea.