Shaka ataka sanaa kutumika kama silaha ya ukombozi wa matatizo ya kijamii

Muktasari:
- Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka ametaka sanaa kutumika kama silaha ya ukombozi wa matatizo ya kijamii na kamwe isiwe chanzo cha mfarakano na vurugu.
Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka ametaka sanaa kutumika kama silaha ya ukombozi wa matatizo ya kijamii na kamwe isiwe chanzo cha mfarakano na vurugu.
Amesema Serikali ya CCM itaendelea kuweka misingi imara ya kuendeleza sanaa hapa nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika jukwaa la wasanii liloandaliwa na kampuni ya Marketing Africa, Shaka amesema wanayo dhamira njema ya kukuza na kuwathamini wasanii.
Amesema dhamira hiyo imejidhihirisha baada ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuanzisha Wizara Maalum ya Sanaa na Utamaduni lengo likiwa ni kushughulikia changamoto za wasanii zilizopigiiwa kelele kwa muda mrefu.
"Tuitumie sanaa kama silaha ya ukombozi wa matatizo ya kijamii na kamwe isiwe chanzo cha mfarakano na vurugu," amesema Shaka.
Ameendelea kusisitiza kuwa Tanzania ni nchi tajiri, yenye rasilimali za kila aina.

"Na rasilimali namba moja ni vipaji vilivyopo hivyo wasanii wakiamua wataweza, kila mmoja wetu ana jukumu la kufanya sanaa yake kwa bidii na maarifa. Na huu ni wakati wa Suluhu, hivyo wasanii wawe wazi kuacha kufanya sanaa kwa mazoea.
"Katika zama tulizonazo, kazi ya sanaa imegeuka kuwa kimbilio kubwa kwa vijana kama sehemu ya soko la ajira hivyo ni wajibu wetu wasanii kuhakikisha kuwa imani ya jamii kwetu inaendelea kwa kulinda mila, desturi na utamaduni wetu," amesema Shaka.
Jukwaa ili limeandaliwa kwa lengo la kutoa elimu ya masoko, uzalishaji bora wa kazi sanaa sambamba na kutoa ushauri wa kibiashara.