Shehena ya madini yanaswa yakisafirishwa kutoka Arusha kwenda Kenya

Pichani ni wafanyakazi wa bus la perfect wakiwa na sehemu ya madini yaliyokamatwa
Muktasari:
Vyombo vya dola nchini Tanzania, vimekamata shehena ya madini kilo 36 zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Arusha kwenda Nairobi nchini Kenya. Uchunguzi unaendelea ili kubaini thamani halisi ya madini hayo
Arusha. Shehena ya madini ya vito aina mbalimbali ikiwepo madini ya Tanzanite imekamatwa ikiwa inasafirishwa kinyume na taratibu kwenda nchi jirani ya Kenya.
Madini hayo zaidi ya kilo 36 yamekamatwa jana Jumatano Juni 26, 2019 na askari maalum ya intelijensia baada ya kupata taarifa madini hayo kutoroshwa kutoka Arusha katika basi la Perfect trans ambalo hufanya safari kutoka Arusha hadi Nairobi nchini Kenya.
Mkuu wa wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe amesema madini hayo ikiwepo Tanzanite kilo tano, Ruby na Greentonaline yalikuwa yanasafirishwa kwenye mfuko mkubwa yakiwa yamechanganywa na mchele.
"Tulipata taarifa za kusafirishwa madini haya na askari wakitumia mbwa waliweza kuyabaini katika gari," amesema
Amesema dereva wa gari hilo na kondakta wake wanashikiliwa kwa mahojiano wakidai hawamjui mmiliki wa madini hayo.
"Wanasema madini walikabidhiwa na mwendesha bodaboda Arusha na kuwa wangefika Namanga (mpakani mwa Tanzania na Kenya) kuna mtu ambaye walipewa namba ya simu angefika kuchukua," amesema.
Hadi usiku kuamkia leo Alhamisi Juni 27, 2019 saa nane maofisa madini mkoa wa Arusha na vyombo vingine vya usalama walikuwa wakiendelea na kazi ya kupima madini hayo ili kujua thamani yake.
Ofisa madini mkazi wa mkoa Arusha, Erick Robert anatarajia kutoa thamani ya madini hayo na aina zake pindi wakikamilisha kuyapima.