Sheikh Mkoa wa Mbeya ataka viongozi wa dini kuliombea Taifa

Waumini wa dini ya kiislamu jijini Mbeya wakiwa tayari kwa ajili ya swala ya Eid El Haji iliyoswaliwa kimkoa kwenye uwanja wa Sokoine jijini humo.Picha na Saddam Sadick

Muktasari:

  • Katika baraza hilo la Eid, Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Akson ameahidi kuchangia mifuko 200 ya saruji, huku Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi akiahidi Sh2 milioni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Bakwata Mkoa huo.

Mbeya. Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Msafiri Njalambaha amewaomba viongozi wa dini nchini kutumia muda wao kuliombea Taifa kuepukana na ugonjwa wa Covid-19 na kuhubiri amani, upendo, umoja na uwajabikaji.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumatano Julai 21, wakati wa swala ya Eid el Adha iliyofanyika kimkoa kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wa Serikali.

Amesema viongozi wa dini zote nchini watumie majukwaa yao kuhimiza amani, upendo na uwajibikaji na kusisitiza kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Covid 19.

 “Tuendelee kuchukua tahadhari kulingana na mwongozo wa watalaamu wanavyotuelekeza, lakini tuilinde amani yetu, tushirikiane, tupendane na tujenge umoja huku tukifanya kazi,” amesema Njalambaha.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Rashid Chuachua ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera amewaomba wazazi na walezi kuwalea vijana wao kimaadili.

Amesema kuwa kwa sasa kumekuwapo na maneno mengi mitaani ambayo siyo ajenda ya nchi na kuwataka kufikiria zaidi miundombinu ya elimu, afya na maji ili kujenga Taifa la maendeleo.

“Tujibidishe zaidi kujenga uchumi, tutengeneze miundombinu ya elimu, afya na maendeleo mengine kwa ujumla, hayo maneno ya mitaani tuyapuuze siyo ajenda ya nchi” amesema Chuachua.