Shemeji mbaroni mauaji ya mchungaji KKKT Iringa

Aron Mkumbo ambaye ni mume wa Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Elizabeth Ng’unga akiwa nyumbani kwake wakati wa mahojiano na mwandishi wa gazeti la Mwananchi. Picha na Tumaini Msowoya

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia Naftari Lulandala (40), mkazi wa Kijiji cha Uhambingeto kwa tuhuma za kumuua shemeji yake, Elizabeth Ng’unga (36).


Iringa. Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia Naftari Lulandala (40), mkazi wa Kijiji cha Uhambingeto kwa tuhuma za kumuua shemeji yake, Elizabeth Ng’unga (36).

Elizabeth, mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, aliuawa Desemba 15, 2021 katika Kijiji cha Kipaduka kisha mwili wake kutupwa kwenye Mlima wa Uhambingeto, wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

Pamoja na kutobolewa macho, mwili wa mchungaji huyo ulikutwa ukiwa umefungwa kwa kamba ya manila shingoni huku mkono wake wa kulia ukiwa majeraha ya kukatwa na kitu chenye ncha kali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa, Alan Bukumbi alisema aliyekamatwa alihusishwa na mauaji hayo ni shemeji yake ambaye mpaka dakika ya mwisho walikuwa pamoja.

Alisema, inadaiwa Mchungaji Elizabeth alienda kwenye kijiji hicho kwa ajili ya shughuli zake za mashamba, kwa kuwa alikuwa analima alizeti.

Alidai akiwa kwenye kijiji hicho alipokewa na mwenyeji wake Naftari ambaye ni shemeji yake kwa maana ya mume wa mdogo wa mchungaji.

“Alikuwa na mwenyeji wake (Naftari) muda wote na hata mashuhuda waliwaona pamoja na bahati nzuri, huyu shemeji mtu ndiye aliyekuja kutoa taarifa Kituo cha Polisi kuwa kuna mama ameuawa,” alisema na kuongeza.

“Maajabu ni kwamba, huyu shemeji yake alipokuja polisi, alisema hamtambui wakati yeye ndiye alimpokea na walikuwa pamoja,” alisema kamanda huyo.

Kamanda alisema inadaiwa mchungaji huyo alikuwa ameuza baadhi ya mazao yake hivyo alikua na fedha zaidi ya Sh2 milioni.

“Kwa hiyo chanzo kikubwa cha mauaji haya ni tamaa ya mali kwa sababu huyu mchungaji alikuwa na fedha ambazo huyu mtuhumiwa alizipora kisha akamuua,” alisema.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, polisi walipofika na kuukuta mwili huo porini, walitangaza eneo hilo wakilenga kuona kama kuna ndugu wakautambue, lakini hakuna mtu aliyejitokeza, hivyo Serikali ya Kijiji ikalazimika kuuzika baada kuona unaanza kuharibika.

Alisema baadaye ndugu walijitokeza na baada ya kufukua kaburi walithibitisha kuwa mwili huo ni wa ndugu yao.

Mama mkwe wa Mchungaji Elizabeth, Anuuza Abeli alisema kinachomuumiza zaidi ni watoto wadogo ambao mkamwana wake amewaacha.

“Wajukuu zangu wadogo sana, mimi naishi Singida nikawa naumwa, hivyo nilikuja hapa kujiuguza, mkamwana wangu aliniita nije lakini nimeishia kulia tu. Sijui nitafanyaje na hawa wajukuu,” alisema huku akilia.

Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Dk Andendekisye Ngogo alisema tukio hilo limewasikitisha na wanaendelea na maombolezo ya mchungaji Elizabeth, nyumbani kwake.

“Kusema kweli ni wajibu wa Kanisa kuhakikisha watoto wa Elizabeth wanatunzwa, mchungaji Elizabeth amefanya kazi kwa miaka tisa. Moja ya mambo tutakayomkumbuka ni umakini wake katika kufanya kazi,” alisema na kuongeza:

“Alikuwa mcheshi na alitamani kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa, tumemkosa Eliza na naamini Mungu atatuletea mbadala wake, jina la Mungu lihimidiwe.”

Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Iringa, Blaston Gavile ndiye aliyetoa taarifa ya awali ya kifo cha Mchungaji Ng’unga ambaye alizikwa rasmi katika makaburi ya Kijiji cha Ilambilole, baada ya mwili wake kufukuliwa alikokuwa amezikwa awali.

Wakizungumzia mauaji hayo, baadhi ya wachungaji wanawake walisema wameumizwa na kwamba, uvivu na tamaa ya mali ndiyo inayosababisha upendo wa jamii kupungua.

“Fikiria pesa kidogo alizokuwa nazo Elizabeth, lakini sisi ni watumishi wa Mungu ambao tunatakiwa kufanya kazi nyingine ili familia zetu ziendelee kutunzwa, sasa kama tukienda shambani tunauawa inakuwaje? Kweli hili limetuumiza sana,” alisema Lukresia Matilibu, mchungaji wa KKKT, Usharika wa Kibwawa.

Mchungaji mstaafu, Esta Chusi alisema amesikitishwa na kifo cha mchungaji huyo ambaye alikuwa kama mwanaye.

“Nimestaafu na nyuma yangu nimewaacha hawa mabinti, fikiria ameuawa akiwa mdogo na watoto wadogo kama hawa najisikiaje? Inaniumiza sana. Mungu mwenyewe aingilie kati,” alisisitiza.