Sherehe, matamasha kusitishwa isipokuwa kwa masharti maalum

Sunday July 25 2021
marufuku pc
By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesitisha rasmi matamasha, sherehe na mikusanyiko ya aina yoyote mpaka pale itakapotangazwa tena, lengo likiwa  kudhibiti mnyororo wa usambaaji wa ugonjwa wa Covid-19 nchini.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Julai 25, 2021 na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi wakati akisoma mwongozo mpya wa kwanza wa kudhibiti misongamano katika jamii bila kuathiri shughuli za kiuchumi.

Amesema shughuli zote zinazokusanya watu ikiwemo baa, kumbi za starehe zinatakiwa kuzingatia miongozo iliyowekwa na Serikali katika kutimiza wajibu wao.

“Sherehe zote kwa kipindi hiki tunasihi sana zisitishwe mpaka pale Watanzania watakavyotangaziwa vinginevyo, suala hili ni la muda na Serikali lengo lake ni kupunguza mnyororo wa maambukizi ya Covid-19.

“Kama ni lazima sherehe zote za harusi zifanyike nje ya kumbi (open air) au kama zinafanyika ukumbini ziwe za muda fupi, wageni waalikwa wawe wachache kuruhusu ukaaji wa mita moja au zaidi.”

Amesema baadhi ya shughuli za kundi hili zinafaa kuangaliwa iwapo ni muhimu? Lazima au zisubiri hali itengamae na iwapo ni muhimu na lazima mambo yafuatayo hayana budi na ni lazima yazingatiwe.

Advertisement

Amesema ni lazima kuwe na kipima joto kwa wote wanaoingia kupata huduma kwenye eneo husika.

"Wamiliki au waandaaji wa mikutano waweke vifaa vya kunawia mikono maji tiririka na sabuni vinavyotosheleza mahitaji au kutumia vipukusi."

Amesema wateja wakae umbali wa mita moja kutoka mmoja hadi mwingine na wengine washauriwe kunywea nyumbani.

Amesema maeneo hayo yakaguliwe na Wataalamu wa Afya na Kamati za Ulinzi na Usalama kuhakikisha maelekezo yanazingatiwa.

Advertisement