Sheria ya dhamana yakosolewa Tume ya Hakijinai

Dar es Salaam. Wakili wa Kujitegemea Zadock Magai amependekeza marekebisho kwenye Kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ili kuipa mahakama mamlaka ya kuamua kutoa au kutokutoa dhamana kwa mshtakiwa.

Wakili Magai ametoa mapendekezo hayo katika Tume ya Hakijinai iliyoundwa na Rais Samia Suhulu Hassan kuangalia namna ya kuboresha mfumo na hakijinai nchini.

Katika mapendekezo yake, Wakili Magai alisema kifungu hicho kinampa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mamlaka ya kuizuia mahakama kutoa dhamana kwa mshtakiwa au mtuhumiwa kwa hati ya maandishi ili kulinda masilahi ya Jamhuri.

“Kifungu hiki kimekuwa kama msitu wa watendaji wa Serikali wasio waaminifu kuwapa watu mashtaka yasiyo na dhamana,” alisema Wakili Magai.

Kifungu hicho alisema kinakinzana na Ibara ya 13(6) ya Katiba hivyo kifanyiwe marekebisho kuipa mamlaka mahakama ya kupima kama mshtakiwa anastahili dhamana au la.

Desemba 22 mwaka 2015 katika hukumu iliyotolewa na majaji wa Mahakama Kuu Shaban Lila (aliyeongoza jopo), Sekieti Kihiyo na Profesa Eudes Ruhangisa walimwondolea DPP mamlaka hayo.

Mahakama ilibatilisha Kifungu cha 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai katika kesi ya kikatiba namba 29 ya mwaka 2015 iliyofunguliwa na Wakili wa Kujitegema, Jeremiah Mtobesya.

Katika kesi hiyo, Mtobesya alikipinga kifungu hicho kwamba kinamnyima mshtakiwa aliye mahakamani au mtuhumiwa aliye polisi haki ya kusikilizwa.

Alisema kila kesi inaangaliwa kwa mazingira yake hivyo kitendo cha DPP kuzuia dhamana kinamnyima haki mhusika n amaelezo kwamba itaathiri masilahi ya umma hayatoshi.

Katika hukumu yake, Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja za Mtobesya kwamba kifungu hicho kinamnyima mtu haki na ni kinyume cha Ibara ya 13 (6) ya Katiba.

Ilisema kifungu hicho kinaenda kinyume cha misingi ya kidemokrasia kwani katika kesi, DPP na mshtakiwa wote wanakuwa na haki sawa lakini kifungu hicho kinaupa upande mmoja mamlaka zaidi na kuondoa mamlaka ya Mahakama kuwasikiliza.

Mwanasheria mkuu wa Serikali hakukubaliana na uamuzi huo hivyo alikata rufaa akiwa na hoja tano lakini tatu ziliondolewa.

Katika hukumu ya rufaa hiyo iliyosomwa Februari 2 mwaka 2018, Mahakama ya Rufani nayo ilizikataa hoja za Serikali ikikubaliana na hoja za Mtobesya na hukumu ya Mahakama Kuu.

“Kwa hiyo Serikali inapaswa ipeleke bungeni marekebisho ya kifungo hicho kama inakubaliana na hukumu ya Mahakama,” alisisitiza Wakili Magai.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama, Moses Ndelwa alisema Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inawapa changamoto na kuchelewesha kesi.

Ingawa mara nyingi watu huilaumu mahakama, alisema mahakama hukosa namna pale upande wa mashtaka unapodai upelelezi haujakamilika jaokuwa huwa inawaachia pale kesi inapochukuwa muda mrefu bila kuendelea lakini hukamatwa tena na kufunguliwa mashtaka hayohayo.

Hivyo, alisema kuna haja ya kuifanyia marekebisho sheria hiyo ili kuweka ukomo wa DPP kumkamata mshtakiwa na kumfugulia mashtaka.