Shinyanga waelimishwa umuhimu waliojifungua kurudi shuleni

Muktasari:
- Wananchi wa mtaa wa Dome Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga wamepewa elimu na hamasa ya kuwapeleka shuleni watoto wa kike waliojifungua ili wakapate haki yao ya elimu baada ya Serikali kuruhusu waliokatisha masomo wakiwamo wasichana waliojifungua kurudi shuleni.
Shinyanga. Wananchi wa mtaa wa Dome Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga wamepewa elimu na hamasa ya kuwapeleka shuleni watoto wa kike waliojifungua ili wakapate haki yao ya elimu baada ya Serikali kuruhusu waliokatisha masomo wakiwamo wasichana waliojifungua kurudi shuleni katika mfumo rasmi.
Hamasa hiyo imetolewa na viongozi wa mtaa huo Januari 10, 2022 kwenye kikao, ambapo wazazi na walezi wenye watoto wa kike waliojifungua majumbani na waliofaulu kuingia kidato cha kwanza wameaswa kutovunjika moyo kuwasomesha watoto wao.
Novemba 2021 aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza rasmi kuwaruhusu wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa kwasababu ya kupata ujauzito wakiwa shuleni kurejea masomoni kupitia mfumo rasmi.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Dome, Solomon Najulwa Akitoa elimu kwa wazazi na walezi aliwakumbusha wazazi kuwa watoto wa kike waliokatishwa masomo kwa sababu mbalimbali wanatakiwa kurudi shule mara moja, ili kuunga juhudi za Serikali.
“Kila mmoja aangalie faida ya kumpeleka shule mtoto wake. Serikali inampango mzuri wa kuwaendeleza watoto hawa, hivyo ni vizuri wazazitukachangamkia fursa ili waweze kupata elimu na watimize ndoto zao" amesema Najulwa.
“Kuna shuhuda nyingi za watoto waliopata ujauzito kwa vishawishi walisoma na walifanikiwa, wengine walibakwa, hivyo wasichana kama hao ukiwaendeleza wanaweza kufika mbali na mzazi akashangaa,” amesema Najulwa.
Kwa upande wake Ofisa Elimu kata ya Ndembezi, Ustadius Mkulu amesema Serikali inapenda kuwaendeleza watoto wa kike ili na wao waweze kutimiza ndoto zao, kwani ni vizuri wazazi wakaona umuhimu wa elimu.
Baadhi ya wazazi walishukuru uongozi wa Serikali kuwakumbusha wajibu wao, kwani kuna wengine walikata tamaa lakini kwa elimu hii watapeleka watoto wa kike na wakiume mashuleni
"Tunashukuru sana mwenyekiti wetu kwa kutupa elimu hii kwani tunaamini Watoto wetu watasoma kwa bidii tutashirikiana na walimu kwa karibu" amesema Yunis Charles