Shule mpya yamaliza hofu ya wanafunzi kushambuliwa na fisi

Muonekano wa miundombinu ya shule mpya inayojengwa katika mtaa wa Nyangaka iliyokaguliwa na mwenge wa uhuru katika halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu. Picha na Samirah Yusuph

Muktasari:

Hofu ya watoto wao kushambuliwa na fisi wakati wa kwenda na kurudi shule ya msingi Kidinda waliokuwa wazazi wa Mtaa wa Nyangaka Wilaya ya Bariadi imeisha baada ya Serikali kujenga shule mpya kwenye mtaa huo.

Bariadi. Hofu ya watoto wao kushambuliwa na fisi wakati wa kwenda na kurudi shule ya msingi Kidinda waliokuwa wazazi wa Mtaa wa Nyangaka Wilaya ya Bariadi imeisha baada ya Serikali kujenga shule mpya kwenye mtaa huo.

Kabla ujenzi wa shule mpya, wanafunzi kutoka mtaa wa Nyangaka walilazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita tano kwenda na kurudi shule ya msingi Kidinda, huku wakiwa na hofu ya kushambuliwa na fisi wanapodamka alfajiri kuwahi shuleni.

Akitoa taarifa ya utekelezaji kwa kiongozi wa bio za Mwenge wa Uhuru, Addalla Shaibu, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kidinda, Charles Sokozi amesema ujenzi wa shule mpya yenye vyumba 16 vya madarasa, matundu 24 ya vyoo na jengo la utawala unatarajiwa kukamilika Julai 30, mwaka huu na itasajili zaidi ya wanafunzi 630.

"Tulipokea Sh540.8 milioni kupitia programu ya Boost kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule mpya yenye mikondo miwili; tayari ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 90," amesema mwalimu Sakozi

Akizungumzia mbio za Mwenge wa Uhuru, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenyeulemavu), Patrobas Katambi amewataka viongozi na watendaji wa halmashauri kusimamia itifaki ya Mwenge ikiwemo kutii na kutekeleza maagizo na maelekezo ya kiongozi wa mbio hizo.

"Wote wanaopuuza au kuonyesha dharau kwa itifaki na maagizo ya viongozi wa Mwenge watachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma,’’ amesema Naibu Waziri huyo