Anusurika kifo kwa kushambuliwa na fisi

Muktasari:
Mkazi wa Kijiji cha Kalangalala Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Moshi Kijimbe (45) amenusurika kifo baada ya kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake na fisi wakati wakitoka matembezi.
Sengerema. Mkazi wa Kijiji cha Kalangalala Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Moshi Kijimbe (45) amenusurika kifo baada ya kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake na fisi wakati wakitoka matembezi.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Julai 20, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Senyi Ngaga amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo ambapo Moshi alifikishwa hospitali ya wilayani humo kwa matibabu.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Sengerema, Sista Mary Jose amethibitisha kumpokea majeruhi huyo ambaye amelazwa wodi namba mbili akipatiwa matibabu na hali yake ikiendelea vizuri.
“Tulimpokea Moshi Kijimbe usiku wa kuamikia leo amejeruhiwa sikio la kulia na mguu wa kulia baada ya kupatiwa matibabu hali yake inaendelea vizuri,”
Mjomba wa Moshi aliyekuwa akimuuguza hospitalini, Masumbuko Deusi amesema alijeruhiwa sikio la kulia na mguu wa kulia ambapo nyama zote zililiwa na fisi huyo kisha kutokomea kusipojulikana.
Mke wa Moshi, Kwili Matayo amesema mume wake anatabia ya kwenda matembezini wakati wa jioni kwa lengo la kubadilishana mawazo na wenzake lakini ilivyofika saa 3 usiku hajarudi nyumbani ikabidi akamtafute.
“Ilipofika majira ya saa 3 usiku hajafika nyumbani niliamua kuchukuwa tochi na kwenda kumfuatilia mume wangu ndipo nilipomkuta akipambana na fisi ili ajiokoe maisha yake, nikaanza kupiga yowe fisi akakimbia akiwa tayari amemjeruhi maeneo mbalimbali ya mwili wake,”amesema Kwili
Ofisa Wanyamapori daraja la ll kutoka kituo kidogo mkoani Mwanza, Mohamed Mpoto amesema wamepata taarifa ya tukio hilo na tayari wametuma timu ya wataalamu kutoka ofisini kwao kwenda kumsaka fisi huyo.
Kijiji cha Kalangalala Kata ya Bitoto ni miongoni mwa vijiji vinavyopakana na Kata ya Tabaruka ambayo wananchi wake wameamua kuchangishwana fedha kwaajili ya kuwawezesha Sungusungu kuwasaka fisi ambao wamekuwa wakisababisha taharuki kwa kushambulia mifugo na kujeruhi wananchi wa kata hiyo.